Thursday, October 29, 2015

ZIJUE FURSA

Nakusalimu ndugu;
Kuna msemo usemao, “Fursa ziko kila mahali zimelala tu ovyo ovyo zikisubiri jicho la kuona zionwe”. Ndugu, najua muda mwingi umekuwa unafikiria ufanye kazi gani itakayokuletea kipato kizuri, tena ikiwezekana kwa muda mfupi. Hili sio wazo lako tu ni wazo la wengi. Inapofika wakati wa kuamua kuanzisha 

biashara au kuwekeza, shida inakuja ni biashara gani ufanye au ni kitu gani uwekeze. Kujiuliza namna ile sio dhambi, ni kawaida kabisa lakini nataka nikueleze kuwa mahali popote ulipo umezungukwa na fursa kibao. Kama hujaziona tatizo sio kwamba fursa hazipo tatizo ni macho yako hayazioni ila zipo. Katika makala hii tutajifunza namna ya kuboresha macho yako na akili yako ili upate nguvu ya kuziona fursa mahali ulipo.

Historia Inatusimulia Kisa Cha Kweli
Tumesoma katika historia kwamba, hapa Tanzania maeneo ya mwambao wa bahari ya Hindi hasa mikoa ya Tanga na Kilimanjaro, wazungu walowezi walikuja kwa lengo la kutafuta fursa. Kwa ustaarabu mkubwa hawakuvamia maeneo hayo bali waliwaona ma-chief wa maeneo husika na waliomba eneo la kuishi kwa muda wakati wakifanya mambo yao. Wale ma-chief kwa hofu ya 

kunyang’anywa ardhi waliwapa wale wazungu maeneo ya milimani yenye mawe ili washindwe kujenga halafu waondoke warudi kwao. Kinyume na matazamio ya wenyeji,baada ya muda wakawaona wale wazungu wamejenga nyumba za mawe huko huko milimani. Kilikuwa sio kitu cha kawaida kujenga nyumba ya mawe kwa wenyeji. Tunapata kujifunza kwamba fursa ziko kila mahali kama huzioni tatizo sio kwamba hazipo, zipo, ila macho yako hayajui kuziona.

Elimu Ya Darasani Inakufundisha Kuona Fursa?
Hatuwezi kujibu swali hili ikiwa hatujaelezana maana ya fursaFursa ni nafasi inayopatikana ambayo ukiitumia vizuri inakuvusha kutoka sehemu moja duni kwenda sehemu nyingine nzuri. Au kwa maneno mengine fursa ni mtu au kitu ambacho ukikitumia vizuri kinakuwa msaada wa kukupatia mafanikio au maendeleo. Tukirudi kwenye swali letu, nakubali kwamba elimu ya darasani, inatufundisha kuona fursa. Kwanza kabisa kusoma  shule ni fursa tayari kwa 

sababu unaweza kupata mafanikio kupitia elimu unayoipata. Tatizo ni moja tu, elimu ya darasani inakufundisha kuona fursa ya aina moja ambayo ni ajira. Watu wengi tuliosoma au wanaosoma shuleni au vyuoni matazamio yao ni kupata ajira. Ni watu wachache ambao wao wanasoma hawana malengo ya kupata ajira bali wanamalengo ya kufanya mambo mengine. Tatizo la kusoma ukiwa na malengo ya kuajiriwa ni kwamba hutaweza kuona fursa nyingine nje 

ya ajira. Utapambana usiku na mchana kutafuta ajira maana ndiyo fursa pekee unayoiona. Mfumo wa kutazamia aina moja tu ya fursa ambayo ni ajira sio mzuri sana, kwa sababu ukikosa ajira unaweza kukaa miaka hata mitano mtaani huku ukilalamika na kulaumu. Kumbe tatizo ni macho yako yamefundishwa kuona fursa moja wakati huku duniani kunafursa maelfu zimetuzunguka kila kona.

Elimu Ya Darasani Inaweza Kukusaidia Au Isikusaidie
Tafiti nyingi zinaonyesha kwamba watu wale ambao hawakuzama sana kwenye mfumo wa elimu ya darasani unaofundisha kuona aina moja ya fursa, wengi wao wanafanikiwa sana kiuchumi. Watu hao wanafanikiwa kwa sababu macho yao wameyazoeza kutazama na kuona fursa nyingi na kwa sababu hiyo kila siku wanaona fursa zimejaa kila kona. Mfano mzuri hapa kwetu Tanzania, Said 

Bakhresa,hakusoma sana, yeye alikuwa na mgahawa wake pale kariakoo, baadaye akapata wazo la kuboresha mgahawa wake, sasa ana viwanda vikubwa vya kila aina. Ana viwanda vya kusindika unga, kusindika maziwa, ana miliki vituo vya luninga, anamiliki timu ya mpira, anasafirisha bidhaa zake na mambo mengine lukuki. Kwake yeye fursa ziko nyingi sana zimejaa kila kona yaani anashindwa  kuzimaliza ingawaje zipo anaziona kila mahali, uwezo unamwishia tu wa kuzifanya zote. Iko mifano ya watu wengi ambao hawakuzama sana 

kwenye mfumo wa kuona fursa moja, baadaye walifanikiwa kwa kiwango kikubwa. Bill Gate alifukuzwa chuoni kisa hana akili leo hii dunia inafurahia kazi yake. Enstein Albert alifukuzwa shule eti sio mbunifu leo hii dunia inashangaa jinsi alivyo na akili nyingi. Sijui kwa upande wako ndugu inawezekana wewe unaona fursa moja au mbili pekee. Mpaka hapo sisemi usisome mpaka elimu ya juu, kama utapata nafasi ya kusoma mpaka mwisho wa elimu kama upo, wewe soma itakusaidia sana kuziona fursa kama utaamua kusaka fursa nyingine.


Mbinu Nne Zitakazokusaidia Kuziona Fursa.

Mbinu ya kwanza: Kuwa Makini (Be Aware). Kama huzioni fursa mpaka sasa unatakiwa kuanzia leo uanze kutazama kwa macho ya kuona fursa. Ili uweze kuziona fursa anza kuwa makini, chochote unachokiona chukua dakika chache kukitafakari huku ukijiuliza hii ni fursa? Ukikuta kuna watu wanalalamikia jambo fulani wewe tafakari hii ni fursa? Kama kuna rafiki yako anakwambia kuna 

jambo la kufanya sehemu fulani wewe tafakari hii ni fursa?. Unapotembea barabarani unakutana na watu wanasema vitu vimepanda bei au vimeshuka bei wewe tafakari hii ni fursa?. Unapangiwa ajira mkoa ambao hukuwa na mategemeo ya kufika huko wakati mwingine ule mkoa hauna mazingira uliyokuwa unayahitaji, usilaumu wewe jiulize hii ni fursa? Kuwa makini namna hii kunakufanya uweze kuziona fursa nyingi ambazo watu wengine hawazioni.

Mbinu ya pili: Kila Unachokiona Kiite Fursa. Mbinu hii ya pili ni nzuri sana itakusaidia kuziona fursa nyingi. Licha ya kuwa makini, kwenye mbinu hii ya pili,kila unachokiona usikione kama kilivyo kione kama fursa yako. Mfano, umehamishwa kiofisi ukapelekwa eneo lingine badala ya kujiuliza uliza uliza 

unatakiwa ujiambie na ujisemee huko ninapopelekwa ni fursa kubwa. Usisikilize maneno ya watu wewe jisemee tu “lazima kutakuwa na fursa nyingi” na kweli ukifika anza kuona kila kitu unachokutana nacho kama fursa. Kwa njia hiyo utaona fursa nyingi sana.

Mbinu ya tatu: Soma Vitabu Ili Uone Fursa Nyingine. Kuwa mpenzi wa kusoma vitabu vingi. Kutoka kwenye vitabu utagundua kuna fursa nyingi sana.

Mbinu ya nne: Kaa Na Watu Wenye Uzoefu Wa Kuona Fursa. Usiogope kuwaona watu wenye upeo mkubwa wa kuona fursa hasa wafanya biashara na wajasiriamali. Mbinu unayoweza kuitumia kuongea naye ni hii: kama unaweza kumwandalia chakula cha mchana au cha jioni andaa, kwa sababu 

unapomwandalia chakula anajisikia vizuri halafu atakupa kila alichonacho kuhusu fursa. Lakini pia unaweza kutumia nafasi hii kumwomba ujiunge naye kwenye biashara yake hata kama bila malipo ili ujifunze. Akikuruhusu hata asipokulipa wewe jitolee  kufanya kazi bure utajifunza mengi, hiyo nayo ni fursa tayari itakusaidia huko mbele ya safari yako.


Share:

0 comments:

Post a Comment

Top Servicare. Powered by Blogger.

Web Design

Popular Posts

INSTAGRAM FEED

@soratemplates

Blog Archive

About