Wednesday, November 4, 2015

Una Uwezo Mkubwa Na Akili Za Kufanya Kile Unachotaka, Vitumie

Habari  mpenzi msomaji wa TOPSERVICECARE. Ni matumaini yangu kuwa mpo salama , ni wakati mwingine tena tunakutana kwa ajili ya kuzidi kujifunza na kukumbushana namna sahihi ya kuangalia mambo. Ndugu yangu napenda nikukumbushe kuwa wewe umeumbwa ukiwa na uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo, ulipewa akili na uwezo wa kufanya kile unatakiwa kufanya hapa duniani.
UNAWEZA.
  
Kuna wakati unakutana na mambo ya kusikitisha na kuumiza pale ambapo mtu anakuwa kama amezipeleka akili zake likizo, au naweza sema amejisahau au kujipoteza kabisa , haelewi hata ni nani, anaenda wapi?, kwa nini yupo? n.k. Baadhi ya watu wapo tu kwa kuwa wapo. Baadhi ya watu hawaelewi hata uwezo walio nao, hawajui kusudi la wao kuwepo hapa duniani, mwingine anafikiri alikuja hapa ili aishie kutamani kuwa kama wengine, hajui kama naye ikiwa atatembea na kukaa kwenye ile nafasi yake anacho kitu cha maana , cha 



kumfanya na wengine watamani kuwa kama yeye, japo ukweli ni kwamba hakuna mtu awaye yote duniani hapa anaweza kuwa kama wewe ndugu yangu, wewe ni wewe, ni wa peke yako, uliumbwa hivyo kwa kusudi maalumu, Kama ulikua haujui hilo ndio nimekujulisha leo na ikiwa ulisahau basi nakukumbusha tu kuwa hakuna aliye kama wewe, usijifananishe na mwingine wala usitamani kuwa kama yule maana hauwezi kuwa vile, utakuwa unajichosha na kujichelewesha kufika kule unaenda tu, tafuta na tamani kuwa kama wewe yule Muumba alikukusudia uwe, tafuta kujua na kuona ule uwezo umeumbwa nao ndugu yangu, tambua zile akili umepewa ndugu yangu. 

Ni jambo la kusikitisha pale unapokutana na mtu anasema kwa kujiamini kabisa kuwa hawezi kufanya jambo fulani na ukitaka kujua ni kwa nini atakuambia eti kwa kuwa fulani alijaribu akashindwa, yaani kwa kuwa tu yule alishindwa naye anaamini atashindwa, anakubali kushindwa bila hata kujaribu kufanya kile kitu, anajipima kwa kumwangalia mtu yule, anajiona yeye hawezi kufanya zaidi ya yule, ndugu yangu tambua kuwa katika maisha haya usitumie kushindwa kwa mwingine kama kipimo cha kwamba nawe huwezi kwenda zaidi ya pale, kwamba hauwezi kufanya zaidi yake, tambua utofauti uliopo miongoni mwetu wanadamu wote, tuna uwezo tofauti wa kufanya mambo, hata namna ya kufikiria tunatofautiana. 




Mwingine anashindwa kwa kuwa tu kachagua kushindwa, ninasema kachagua kushindwa kwa maana ya kwamba kama mtu unatumia kigezo cha kwamba kama na yule kashindwa basi na mimi siwezi, mtu huyu ameamua na kuchagua kushindwa lakini angeamua kuangalia kushindwa kwa mwenzie kwa namna tofauti angeweza kufanya vizuri zaidi. Badala ya kukubali kushindwa kwa kuwa yule kashindwa au alishindwa unaweza kuamua kumfuata yule aliyeshindwa na uweze kuchunguza na kuelewa ni kwa nini alishindwa na kuanzia hapo unaweza kupata vitu vya kukufanya wewe hata ukiamua kufanya hilo ufanye kwa uzuri na usahihi zaidi, maana unajua wapi mwenzio aliangukia, unakuwa na nafasi ya kurekebisha. 

Lakini pia ukitambua kuwa wanadamu tunaomba mambo yale yale kwa utofauti hautalinganisha uwezo wako na wa yule, utatambua kuwa wewe ni wewe na yule ni yule, lakini ukielewa kuwa muumba wako amekupa uwezo , akili na nguvu za kufanya kile anataka ufanye hautajilinganisha na wengine, hautajipima kwa kuangalia yule kafanya nini. Maana cha muhimu ni wewe kutambua uwezo wako, nafasi yako na kusimama hapo, kufanya kila jambo kuendana na nafasi yako, kujiona wewe kama wewe na kuona kuwa unao uwezo wa kufanya kile umeumbwa uje kufanya, ni vyema kuuliza, kuomba ushauri kwa wengine lakini katika hayo usisahau akili zako, au kuna ule usemi unasema ukiambiwa changanya na zako, pima , jihoji angalia kama ni kweli, kinafaa kwako, usiwe ni mtu wa ndio kila wakati, chunguza mambo, pima, amua. 



Ndugu yangu hata ukiambiwa kitu usiwe ni mtu wa kukubali tu, kubali ikiwa kweli kinakubalika na una sababu ya msingi ya kukubali ikiwa kinyume kuwa mkweli na uonyeshe kile unaona na kuamini, usiogope kusema ukweli, usiogope kusimamia kile akili yako inakuridhisha kuwa ni kweli na sahihi hata kama hakuna mtu anayekuelewa lakini ikiwa dhamiri yako haikuhukumu uwe na amani na kusimamia hapo, usifanye jambo kwa kufuata mkumbo, fanya kwa kuwa una uhakika ndicho kitu unahitaji na ni kitu sahihi. 


Share:

ZIJUE FAIDA NNE ZA KUJENGA NYUMBA KWA KUTUMIA RAMANI YA NYUMBA


Ramani ni neno lililozoeleka masikioni mwa watu wengi kwa waliosomea fani hiyo ya ramani na hata kwa watu ambao hawajasomea fani hiyo kutokana na ukweli kwamba ramani hutumika kila siku katika maisha yetu ya kila siku na hakuna uwezekano wa kulipinga hili.

Mfano: Wewe ni mwenyeji katika eneo fulani na unamfahamu mzee mmoja katika eneo hilo anaitwa Mzee Mwamba, basi mara ukakutana na mtu mmoja akakauulizia kuhusu mzee huyo na akakuomba umwelekeze mahali anapoishi mzee huyo, bila shaka utaanza kumwelekeza: nyooka na barabara hii kama mita hamsini hivi mbele utaona barabara inakunja kona kuelekea kulia nenda nayo hiyo barabara kama mita miambili hivi utaona jengo kubwa jeupe mkono wa kushoto halafu mkabala na jengo hilo utaona  duka la vifaa vya ujenzi, uliza hapo dukani watakuonesha nyumba ya huyo mzee.


Hayo maelekezo uliyoyatoa ni ramani sema tu hujaichora na ukiamua kuichora utaiona kama zilivyo ramani za kawaida.
Kwa mantiki hiyo kila mtu kichwani mwake ana ramani nyingi sana nzuri zenye manufaa kwake na kwa taifa kwa ujumla na laiti ramani hizo zingechorwa  tungekuwa na maktaba kubwa ajabu na wakati mwingne hata sehemu ya kuhifadhi zisingetosha.

Maisha ya kila siku.
Unapotaka kuishi kwako yaani katika nyumba yako mwenyewe kuna ramani ya nyumba yako ungependa iwe yaani mwonekano, rangi, ukubwa na hata mwelekeo (orientation) wake. Ungependa umpate mtu mwenye uwezo wa kuionesha ramani hiyo iliyoko kichwani mwako na kisha uipate na uanze hatua  ya kuijenga ili uipate ile furaha unayodhani utaipata mara nyumba hiyo itakapo kamilika.



Itakusaidia kukadria gharama za ujenzi.
Maadamu  ramani hiyo itakuwa imeonesha vipimo vya “material” ya ujenzi itakuwa rahisi kujua idadi ya bati, matofali, madirisha,nk hii itasaidia kukufanya ujipange vizuri kabla ya kuanza ujenzi.

Ni kiambatisho muhimu katika kupata kibali cha ujenzi.
Kwa mujibu wa sheria ya ujenzi wa majengo  inataka ili mtu apate kibali cha ujenzi wa jengo lolote ni lazima aambatanishe katika maombi yake ramani ya jengo analotaka kujenga. Ramani hii itasainiwa na Afisa mipango miji, afisa ardhi na bwana afya na kamati ya ujenzi ya wilaya/mji/manispaa/jiji. nk

Ramani ya nyumba ni kielelezo muhimu katika taasisi za mikopo.
Ukitaka kuchukua mkopo benki au katika taasisi za mikopo na hasa ukitaka kuweka nyumba kama dhamana watahitaji kuiona ramani ya nyumba yako na watahitaji kuiambatanisha katika barua yako ya maombi ya mkopo huo.

Hizo ndizo faida kuu nne za kujenga nyumba kwa kutumia ramani ya nyumba ingawaje zinaweza kuwepo nyingine nyingi, ikumbukwe kuwa kujenga nyumba bila ramani ni sawa na kulima shamba kubwa bila kujua utapanda nini katika shamba hilo, ni hatarii.






TOPSERVICECARE tunaamini kuwa “Kile akili ya binadamu inakiwaza na kukiamini, akili ya binadamu inaweza kukipata”.Na tena, Mtu mmoja mwenye ujasiri ni watu wengi


Tunakuhamasisha ili ufikie mafanikio yako
Share:

NAMNA YA KUPATA KIBALI CHA UJENZI WA NYUMBA ILI USIJE UKAPIGWA STOP WAKATI WA UJENZI WA NYUMBA YAKO



Kutokana na kuongezeka kwa ujenzi holela sehemu za mijini, Serikali iliamua kuandaa sheria ya mipango miji inaitwa “Sheria ya Mipango Miji namba 8 ya mwaka 2007”. Sheria hiyo inaelekeza namna ya upangaji wa miji.  Moja ya maagizo ya sheria hiyo inamtaka kila mtu anayejenga nyumba kwenye eneo liliotangazwa kuwa eneo la mipango miji awe na kibali cha ujenzi na asipokuwa na kibali hicho hatua zaidi huchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa kujenga.
Kwa kufuata maagizo ya sheria hiyo kila halmashauri nchini huandaa sheria ndogo ndogo (by laws) za namna ya utoaji wa kibali hicho cha ujenzi. Sheria hizi ndogo ndogo  hutofautiana kutoka halmashauri moja hadi nyingine. Lakini angalau huwa kuna mlolongo unaokaribiana katika utoaji kibali hicho. Nachukua nafasi hii kukushrikisha mlolongo (hatua) za kupata kibali hicho.

Hatua ya kwanza: Andaa Ramani Ya Nyumba Utakayoijenga
Unatakiwa kuwa na ramani ya nyumba utakayo ijenga. Ramani unaweza kuipata kwa mtu yeyote anayechora ramani za nyumba mfano anaweza kuwa Msanifu ramani, au Msanifu Majengo anaweza kukuchorea ramani nzuri.



Hatua Ya Pili: Ramani Hiyo Inatakiwa Kuidhinishwa Na Msanifu Majengo (Architect) Aliyesajiliwa.
Lengo la Msanifu Majengo kuiidhinisha ramani hiyo ni ili kuangalia ubora na vigezo muhimu vinavyotakiwa kwenye nyumba. Pia likitokea tatizo kwenye nyumba hiyo Archtect atawajibika kujibu ikiwa tatizo hilo litatokana na kosa la mchoro wa nyumba hiyo. Wasanifu majengo waliosajiriwa wako wengi kwenye kila mkoa. Ulizia tu utawapata, kinachotakiwa Msanifu majengo huyo atapiga mhuri wake aliopewa na Bodi ya usajiri wa wasanifu majengo kwenye kila ukurasa wa ramani hiyo.
Huwa kuna gharama kidogo kwenye kuidhinisha ramani kwa architect kulingana na aina ya ramani, mfano kama ni ramani ya nyumba ya kuishi yenye vyumba vitatu au vine kuna wengine huwa wanafanya shilingi 50,000/= na wakati mwingine huwa zaidi ya hapo.

Hatua Ya Tatu: Chukua Fomu Kutoka Ofisi Ya Ujenzi Na Uzipitishe Zisainiwe Kila Sehemu Inayohitajika
Fomu hizi zinatakiwa zipitishwe kwa Afisa Ardhi wa Wilaya husika, kwa Afisa Mipango Miji na kwa Bwana Afya wa Wilaya. Sehemu hizo zote kila mmoja atakagua mambo yake. mfano, Afisa Ardhi atakagua kama kiwanja kinamilikiwa kihalali na kinalipiwa kodi ndio maana unatakiwa uambatanishe na Hati au Offer ya kumiliki kiwanja na risiti ya malipo ya kodi ya kiwanja ya hivi karibuni.

Afisa Mipango Miji atakagua aina ya nyumba unayotaka kujenga na matumizi yake na atalinganisha kwenye ramani ya mipango miji ajue eneo unalotaka kujenga hiyo nyumba linepangiwa matumizi gani. Kama eneo unalotaka kujenga limetengwa kwa ajili ya viwanda na wewe unataka kujenga nyumba ya makazi hata kubali kusaini kwenye sehemu yake. Bwana Afya atakagua ukubwa wa madirisha na uhusiano wa matumizi ya chumba kimoja na kingine. Pia atakagua shimo la maji taka (septic tank). Ukimaliza kupitisha huko utairudisha fomu hiyo ofisi ya ujenzi.

Hatua Ya Nne: Kutembelea Kiwanja Na Kujiridhisha.
Baada ya hapo Mhandisi wa Ujenzi itabidi uende naye kwenye kiwanja unachotaka kujenga ili akajaze taarifa za kiwanja chako na akajiridhishe kama kiwanja kweli kipo. Taarifa ya kiwanja chako atazijaza kwenye fomu hizo kuna sehemu ya kujaza Mhandisi wa Ujenzi. Halafu atapiga mhuri wa ofisi ya ujenzi kama ishara ya kwamba kila kitu kiko vizuri.

Hatua Ya Tano: Kuidhinishwa Na Kamati Ya Ujenzi Ya Wilaya Husika.
Mhandisi wa ujenzi akisha kagua kiwanja chako na akajaza taarifa zake kwenye fomu, kinachofuata ramani hiyo na fomu zote itapelekwa kwenye kikao cha kamati ya ujenzi ya Wilaya ambacho hukaa mara moja kila baada ya muda fulani mfano kuna baadhi ya halmashauri kamati hiyo hufanya kikao chake kila baada ya miezi mitatu. Kikao hicho ndicho kitaidhinisha kutolewa kwa kibali cha ujenzi wa nyumba unayotaka kujenga.

Hatua Ya Sita: Kibali Kinatolewa.
Mara baada ya kikao cha kamati ya ujenzi kumalizika, vibali vyote vilivyoidhinishwa kutolewa, hutolewa kwa wahusika. Kinachotakiwa wakati wa mchakato wote huo uwe na nakala 3 au 4 za ramani yako ya nyumba ili mara baada ya kutolewa kwa kibali cha ujenzi nakala moja atabaki nayo mwenye nyumba, nakala nyingine itapelekwa Ofisi ya Ardhi ya wilaya na nakala moja itabaki kwenye Ofisi ya Ujenzi kama kumbukumbu.
Ukipata kibali chako unaweza kuendelea na ujenzi wako kwa amani bila bughuza. Kutokuwa na kibali cha ujenzi ukibainika unaweza kuzuiliwa kujenga (stop order) mpaka utakapopata kibali cha ujenzi.


“Moja ya maagizo ya sheria hiyo inamtaka kila mtu anayejenga nyumba kwenye eneo liliotangazwa kuwa eneo la mipango miji awe na kibali cha ujenzi na asipokuwa na kibali hicho hatua zaidi huchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa kujenga

Tunakutakia kila la heri katika ujenzi wa Taifa. TOPSERVICECARE
Share:

Saturday, October 31, 2015

Hizi ndizo faida 50 za mazoezi

Moja ya mahitaji matano (5) mhimu ili kuishi baada ya oksijeni, majichumvi, na potasiamu; ni Mazoezi. Mazoezi ni mhimu kwa ajili ya afya zaidi ya kuwa na maumbile ya kuvutia (sex body), burudani au kitu kingine chochote.
Watu wengi hufuatilia kuhusu chakula tu, hata kama utakula vizuri vipi bila mazoezi mlo haujakamilika, kwa hiyo mazoezi ni mhimu kwa yeyote kama ilivyo kwa maji au chakula.

Hizi ndizo faida 50 za mazoezi

Zifuatazo ni moja ya sababu 50 mhimu za kufanya mazoezi kwa afya bora na maisha marefu bila maumivu:
1. Hukufanya ujisikie vizuri
2. Huongeza uwezo wa kujifunza
3. Hujenga uwezo wa kujistahi
4. Huongeza nguvu ya ubongo kufanya kazi
5. Huuweka mwili wako kuwa unaofaa (fit) na wenye uwezo
6. Huongeza afya ya akili yako
7. Huongeza kinga ya mwili
8. Hupunguza mfadhaiko/stress
9. Hukufanya ujisikie vizuri/mwenye furaha
10. Hukufanya usizeeke mapema
11. Huweka ngozi yenye mng’aro na yenye afya
12. Husaidia kupata usingizi mtulivu
13. Husaidia kuzuia ugonjwa wa kiharusi/strokes
14. Huongeza ufanisi katika makutano/joints ya mwili
15. Huongeza nguvu za mishipa
16. Huondoa wasiwasi
17. Huongeza kumbukumbu
18. Husaidia kudhibiti ulevi/uteja
19. Huongeza uzarishaji
20. Huongeza uwezo wa ubunifu
21. Hupendezesha muonekano wa mwili
22. Huongeza uwezo wa kujiamini
23. Husaidia kuongeza nguvu juu ya malengo yako maishani
24. Huondoa tatizo la kukinaishwa na chakula
25. Huongeza miaka ya kuishi
26. Hukomaza mifupa
27. Huongeza afya ya moyo
28. Huongeza hali ya kuwa na msimamo
29. Huondoa homa ndogo ndogo mwilini
30. Huongeza hamu ya kula
31. Hudhibiti usawa wa lehemu/kolesteroli
32. Hupunguza uwezekano wa kupatwa na baadhi ya kansa
33. Hushusha shinikizo la juu la damu/BP
34. Hupunguza uwezekano wa kupatwa na kisukari
35. Huzuia kupatwa na ukichaa/uwendawazimu
36. Hupunguza au huzuia maumivu ya mgongo
37. Hupunguza uwezekano wa kupatwa na ugonjwa wa mifupa
38. Hupunguza hisia/fikra za kujisikia vibaya au huzuni
39. Huzuia kupotea kwa mishipa
40. Huongeza nguvu na ustahimilivu
41. Huongeza ufanisi katika michezo
42. Huongeza uwezo wa kuvumilia maumivu
43. Huongeza usawa na ushirikiano wa mwili
44. Huongeza usambazaji wa oksijeni katika seli za mwili
45. Huongeza hali ya ufuatiliaji/concentration
46. Huongeza uwezo wa kujitawala na kujidhibiti nafsi
47. Huondoa uchovu
48. Huongeza nguvu katika tendo la ndoa
49. Hufanya maisha ni yenye kuvutia zaidi
50. Huongeza ubora wa maisha
Mazoezi yafuatayo ni mazuri sababu ya thamani yake ya baadaye na hayasababishi maumivu kwenye maungio, nayo ni; kutembea kwa miguu, kuogelea, kuendesha baiskeli, kucheza tenisi, gofu, kukwea, kudansi na kadharika.
Share:

Kitunguu Swaumu hutibu magonjwa 30

MUNGU anaposema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa hamaanishi maarifa ya kutengeneza au kuendesha ndege, ni maarifa ya kawaida tu katika maisha yetu ya kila siku ambayo yanaweza kubadilisha afya na ustawi wetu. Moja ya mmea ambao umependelewa sana na Mungu kwakuwa na viinilishe vingi na mhimu sana kwa afya ya binadamu ni kitunguu swaumu. Kitunguu swaumu ni dawa karibu kwa kila ugonjwa.
Huko sokoni tayari nimeviona vitunguu swaumu kutoka China na Afrika kusini ambavyo vyenyewe huwa vina punje kubwa nene na huwa rahisi kuvimenya, hata hivyo ili upate faida hizi zote hapa chini naendelea kukushauri utumie vitunguu swaumu vyetu vinavyolimwa hapa Tanzania kwani hivyo vya kutoka nje pamoja na kuwa ni rahisi kuvimenya lakini ubora wake si kama ule wa vitunguu vyetu.
Hakikisha kila mboga unayopika haikosi kitunguu swaumu ndani yake na ikibidi ukiweke mwishoni mwishoni unapokaribia kuipuwa mboga yako toka katika moto kwamba kisiive sana hata kupoteza viinilishe vyake. Kama una friza au friji ya kawaida unaweza kumenya vitunguu swaumu hata kilo nzima na kuvitwanga kidogo katika kinu, vifunge vizuri katika bakuli au mfuko wa plastiki na uvihifadhi katika friza au friji na hivyo kila unapopika unachukuwa tu na kukitumia ili kuepuka usumbufu wa kukimenya kila siku.
Lakini ili upate faida zaidi za kitunguu swaumu utatakiwa ukimeze katika majikikiwa kibichi, yaani bila kupitishwa katika moto au kuwa kimepikwa.
Chukuwa kitunguu swaumu kimoja
kitunguu swaumu
kitunguu swaumu

Kigawanyishe katika punje punje
kitunguu swaumu
kitunguu swaumu

Menya nusu yake (punje 8 au 10 hivi),
kitunguu swaumu
kitunguu swaumu

Menya punje moja baada ya nyingine
kitunguu swaumu
kitunguu swaumu

Kisha vikatekate (chop) vipande vidogo vidogo na kisu
kitunguu swaumu
kitunguu swaumu
Meza kama unavyomeza dawa na maji vikombe 2 kila unapoenda kulala au fanya kutwa mara 2 kama unaumwa na moja wapo ya magonjwa niliyoyaorodhesha hapa chini.
Fanya hivi kila siku au kila mara unapopata nafasi na hivyo utakuwa mbali na kuuguwauguwa. Mama mjamzito chini ya miezi 4 ni vema asitumie, kwa ujumla tu mjamzito uwe makini utakapotumia kitunguu swaumu kwa namna hii kama wewe ni mjamzito.
kitunguu swaumu
Kitunguu swaumu kilichokatwakatwa/chopped

Kitunguu swaumu hutibu magonjwa 30

Haya ni baadhi ya magonjwa yanayotibika au kukingika na kitunguu swaumu:
  1. Huondoa sumu mwilini
  2. Husafisha tumbo
  3. Huyeyusha mafuta mwilini (kolestro)
  4. Husafisha njia ya mkojo
  5. Hutibu amoeba, minyoo na Bakteria
  6. Huzuia kuhara damu (Dysentery)
  7. Huondoa Gesi tumboni
  8. Hutibu msokoto wa tumbo
  9. Hutibu Typhoid
  10. Huondoa mabaka mabaka kwenye ngozi
  11. Hutibu mafua na malaria
  12. Hutibu kifua kikuu
  13. Hutibu kipindupindu
  14. Hutibu upele
  15. Huvunjavunja mawe katika figo
  16. Hutibu mba kichwani
  17. Huupa nguvu ubongo
  18. Huzuia meno kung’ooka na kutuliza maumivu
  19. Huongeza SANA nguvu za kiume
  20. Hutibu maumivu ya kichwa
  21. Hutibu kizunguzungu
  22. Hutibu shinikizo la juu la damu
  23. Huzuia saratani/kansa
  24. Hutibu maumivu ya jongo/gout
  25. Huuongezea nguvu mfumo wa mmeng’enyo wa chakula
  26. Huongeza hamu ya kula
  27. Huzuia damu kuganda
  28. Husaidia kutibu kisukari
  29. Husaidia kutibu tatizo la kukosa usingizi
  30. Huongeza SANA kinga ya mwili
Share:

UFAHAMU WAKATI MZURI WA KUPATA MAWAZO MAPYA NA KUJIONA MWENYEWE

Habari Ndugu:
Katika maisha yako umesha chunguza na ukafahamu ni wakati gani huwa unapata mawazo mapya au ni wakati gani huwa unajisikia furaha utulivu wa akili na hatimaye unapata nguvu mpya ya kusonga mbele kwenye maisha yako? Je, ni wakati ukiwa umelala?, ni wakati ukiwa unaangalia mpira?, ni wakati ukiwa na rafiki yako? Ni wakati ukiwa baa? Au ni wakati gani?
Dunia imejaa kelele nyingi kila mahali, kuna kelele za magari, kuna kelele za watu, kuna kelele za mihemko ya mwili na kuna kelele za wanyama na ndege 

wa angani. Tunayo bahati kubwa sana miili yetu inauwezo wa kuchuja hizo kelele na hatimaye hazikuathiri sana lakini katikati ya kelele hizo  ni vigumu sana kupata wazo jipya na kujiona mwenyewe. Pia katikati ya kelele hizo ni vigumu sana kupata nguvu mpya.
Kuna rafiki yangu mmoja nilimwuliza hivi;  “Ni wakati gani huwa unapata mawazo mapya?” “Akasema kwa kweli mara nyingi sana nikiwa naangalia mpira huwa napata mawazo mapya na siku nyingine nikiwa napiga stori na marafiki zangu huwa napata mawazo mapya”.
Nikamwuliza kwa namna hii “Ni wakati gani huwa unajiona mwenyewe? Akashangaa! kujiona mwenyewe? Mbona kila siku huwa najiona hata sasa najiona au unamaanisha nini? Nikamwambia sina maana nyingine ni hiyo hiyo ni wakati gani huwa unajiona mwenyewe? Akasema hapo sijakuelewa naomba ufafanuzi.


Nikaanza kumweleza; mara nyingi sana sisi binadamu huwa hatujioni sisi mwenyewe lakini huwa tunawaona watu wengine, pale wanapofanya mambo mazuri wakati mwingine huwa wa kwanza kutoa maoni yetu juu ya mafanikio hayo au wanapofanya vibaya huwa vile vile wa kwanza kutoa maoni yetu juu ya kufanya vibaya kwao. Wakati tunatoa maoni yetu juu ya watu wengine macho yetu na akili zetu huwa zinasahau kujiona (kujiangalia) sisi wenyewe. Kwahiyo kujiona wewe mwenyewe (finding yourself) ni kule kujitambua kutoka ndani 

yako sehemu ulipo katika mambo yote, mfano kiuchumi, kiroho, kielimu n.k
Mtu anayejiona yeye mwenyewe anakuwa makini na anakuwa na kiu ya kutaka afike sehemu fulani, hapotezi muda bure kwenye mambo yasiyomsaidia kwenye maisha yake, tena mtu anayejiona yeye mwenyewe sio mwepesi wa kutoa maoni juu ya watu wengine maana kabla hajatoa maoni juu ya watu wengine jicho lake litamwona yeye kwanza. Baada ya maelezo hayo akasema hapo nimekuelewa.
Ninachotaka nikushirikishe ndugu kwenye makala hii ni kwamba  kuna wakati ambapo mtu anaweza kujiona yeye mwenyewe wakati huu anapojiona yeye mwenyewe ndipo anapata mawazo mapya yenye kumjenga. Je, ni wakati gani huo?


Ni wakati wa KUPUNGA. Kupunga ndio nini? Kupunga ni wakati ambapo mtu anaenda sehemu tulivu yenye mandhari nzuri na mara nyingi wakati wa jioni au mchana kwa lengo la kutafakari. Mtu huenda kwenye eneo hilo akiwa peke yake. Kupunga ni namna ya kupata mawazo mapya na kujiona wewe mwenyewe na njia hii ilitumiwa tangu enzi za mababu wa kale na kale. Walikuwa wanatumia njia hii ya kupunga kondeni hasa mara baada ya kazi ngumu. Baadaye katika kizazi chetu watu wameanzisha utaratibu wa kwenda 

kupunga na marafiki zao sehemu za fukwe ya bahari au ziwa.
Lakini kupunga yenye lengo la kupata mawazo mapya na kujiona wewe mwenyewe unatakiwa uwe peke yako ukitafakari jinsi ulivyo, maisha yako yalivyo, mwelekeo wako utakuwaje lakini pia ukifurahia mandhari nzuri ya uso wa dunia na wakati mwingine miziki ya sauti za ndege ikiimba kwa mbali. Wafalme wengi walitumia njia hii ya kupunga ili kupata utulivu wa akili na utulivu wa moyo katika kutawala kwao na  jinsi ya kukabiliana na maadui zao.

Je, wewe huwa unapunga?. Kuna faida nyingi sana za kupunga, mimi baada ya kuzifahamu faida hizo mara nyingi huwa napunga. Utanikuta niko sehemu tulivu yenye mandhari nzuri au wakati mwingine huwa naenda mlimani napanda juu ya mlima halafu naanza kufurahia jinsi dunia ilivyo nzuri, jinsi mimi mwenyewe nilivyo mzuri, si hayo tu bali huwa napata msimamo wa maisha yangu. Toka nikiwa kidato cha kwanza nilianza tabia hii ya kupunga mpaka sasa naendelea, kwa kweli ni furaha kubwa. Naomba nikushirikishe baadhi ya faida unazozipata kwa kupunga.

Kubadili msimamo hasi wa kimawazo.
Kupitia kupunga huwa nabadilika kabisa jinsi ya kufikiri kwangu, wakati mwingine huwa moyoni nimejaa fikira potofu za mahangaiko ya hapa na pale lakini nikienda kupunga nguvu mpya hunijia na  mawazo mapya ya kukabiliana na changamoto za maisha yaninijia.

Kupata furaha na raha ya kuishi duniani.
Ni kweli kabisa kama nilivyokudokeza hapo mwanzo, wafalme wengi na mpaka hivi sasa utakuta wana bustani kubwa na nzuri mara nyingi saa za jioni huenda 

kwenye bustani zao na kufurahia maisha. Mara nyingi mimi nikiwa napunga huwa nafurahi sana kuona mimi ni mzima mwenye afya na huwa nafurahi sana kuona dunia jinsi ilivyo nzuri. Zaidi ya yote huwa nafurahi sana ninapowasikia na kuowaona ndege jinsi wanavyoimba na kufurahi. Nikiwa napungia ufukweni huwa nafurahi sana kuona jinsi bahari au ziwa linavyopendeza na wakati mwingine nikiwaona viumbe vya bahari wanavyofurahia maisha wakiruka ruka kwenye ulimwengu wao.

Kutoa wivu, hasira na kujaa upendo.
Wakati mwingine huwa tunakwazwa na mambo mengi sana katika maisha. Ukiwa na tabia ya kupunga utashangaa hizo sumu zinatoweka na badala ya kuwa na hizo sumu unakuwa na upendo mwingi. Kwanza unajipenda wewe mwenyewe na unajiona ni mwenye bahati. Lakini pia kama utakuwa unapungia eneo lenye ndege au wanyama, viumbe hao watakufundisha jinsi wanavyoishi kwa kupendana wakifurahi siku zote.

Kujiona wewe mwenyewe.
Hili ndilo lengo hasa la makala hii, wakati wa kupunga ni wakati wa kujiona wewe mwenyewe. Ndio maana nakushauri unapopunga kwa lengo la kujiona wewe mwenyewe unatakiwa uwe peke yako. Wakati ukiwa unatafakari tafakari utashangaa utakapojiona wewe mwenyewe jinsi ulivyo mzuri, ulivyo barikiwa, tena utajiona wewe mwenyewe jinsi unavyotakiwa kuongeza juhudi kwenye mambo yako mazuri nk. Unapokuwa kwenye kelele nyingi sio rahisi kujiona wewe mwenyewe wala hutajigundua jinsi ulivyo. Nakushauri kama unanafasi anza tabia hii ya kupunga utashangaa jinsi utakavyojiona wewe mwenyewe.

Unapokuwa unapunga ufanye nini zaidi?
Unapopunga unatakiwa kuwa kwenye eneo lenye utulivu, ni vizuri ukazima simu yako ili ubaki peke yako. Unapopunga jifurahie wewe mwenyewe, pumua kwa nguvu halafu jisikilizie jinsi ilivyo raha kupumua, utashangaa wakati unapumua kwa namna hii utaona kila kitu kinachokuzunguka jinsi kilivyo kizuri, anga litakuwa zuri miali ya mwanga itakuwa inadunda dunda hata hakuna lugha ya kuielezea.

Ushauri wangu.
Mpendwa msomaji wa Top Service Care nakushauri anza kuwa na tabia ya kupunga angalau tenga hata siku moja kwa wiki saa ya jioni mara baada ya kazi nenda kwenye eneo zuri ukapunge. Kunafaida kubwa sana ya kupunga hata Mungu mwenyewe huwa anapunga saa ya jioni kama ilivyoandikwa kwenye 

kitabu cha Mwanzo. Mimi naamini nguvu iliyomo wakati wa kupunga, na nitaendelea siku zote kupunga nipatapo nafasi. Kama hujaanza wala hujawahi kujaribu basi mara umalizapo kusoma makala hii jiwekee ratiba ya kupunga halafu utaniambia jinsi ilivyo raha kupunga. Unaweza kuniandikia kwa email
“Kupunga ni namna ya kupata mawazo mapya na kujiona wewe mwenyewe na njia hii ilitumiwa tangu enzi za mababu wa kale na kale. Walikuwa wanatumia njia hii ya kupunga kondeni hasa mara baada ya kazi ngumu”

Tunakuhamasisha ili ufikie mafanikio yako
Share:

UNAPOIHARIBU NAFSI YAKO

Habari yako ndugu na rafiki yangu;
Ninakukaribisha katika tafakari yetu ya leo, ambapo nimekuwa nikikuletea makala hizi kwa lengo la kukusaidia pale unapokwama ili kwa pamoja tusonge mbele katika maisha yetu na lengo langu kubwa ni ili mimi na wewe tufanikiwe. Masomo haya ninayokuletea haya kusaidii wewe tu wala siandiki ili nikufundishe wewe tu, kati ya watu wanaofaidika zaidi na masomo haya ni mimi mwenyewe yananifundisha mambo mengi sana na yananisaidia mambo mengi mno. Huwa na kaa na kutulia naanza kuzisoma makala hizi nilizoziandika mimi mwenyewe 

halafu najifunza mambo mengi ambayo yananisaidia kila siku kwenye harakati zangu za mafanikio. Kwa sababu mafanikio ni vizuri kumshirikisha  mwenzako ndio maana nakushirikisha wewe ili upate kufaidika na hatimaye ufikie mafanikio yako. Mfano mzuri, mwezi wa tano mwaka huu (2015)  nilipata fursa moja ya kujiunga na rafiki zangu wanne ili tuanzishe ufugaji wa kuku. Nilikuwa natakiwa kuchangia shilingi milioni mbili kwenye mradi huo. Kwa wakati huo 

sikuwa na pesa yoyote wala sikujua nitapata wapi pesa hizo. Wakati natafakari hayo nikakumbuka makala moja niliiandika kipindi cha nyuma kidogo yenye kichwa cha habari; Jinsi Ya Kupata Chochote UnachokitakaHaraka haraka nikakimbilia kuisoma makala hiyo, mara nilipomaliza kuisoma nikapata akili nikaanza kuyatumia mafunzo niliyojifunza humo. Baada ya siku mbili nilipata milioni mbili. Nilishangaa sana ndipo nikaelewa kuwa makala hizi ninazoziandika sio kwa ajili yako tu bali pia kwa ajili yangu.

Mara nyingi sana ninapokumbana na tatizo au changamoto fulani huwa natumia makala zangu kama washauri wangu na zimenisaidia sana siku kwa siku. Hivi karibuni nilikuletea makala nyingine yenye kichwa cha habari; Kukiomba Msamaha Kila Kiungo Cha Mwili Wako Ni Siri YaAjabu Kukutoa Kwenye Tabia Sugu. Wakati naendelea kuyafanyia kazi mafunzo yaliyomo kwenye makala hiyo, nimekuja kugundua kwamba usiporekebisha baadhi ya mwenendo wa maisha yako hutaweza kamwe kujinasua na tabia sugu. Tabia sugu maana yake 

ni mwenendo na matendo ambayo umekuwa ukiyafanya, lakini hupendi uyafanye kwa sababu yanakuharibia maisha yako, tena yanakupotezea muda, kibaya zaidi yanakurudisha nyuma kwenye harakati zako za kuelekea mafanikio makubwa. Pamoja na ubaya wa hiyo tabia sugu kwako, bado huwezi kuiacha au unajaribu kuiacha lakini unajikuta umerudia tena. Mfano wa tabia sugu inaweza kuwa ni uvivu, unajitahidi uache uvivu lakini bado unashindwa kuacha, unajikuta unaendelea kulala au kupiga soga mpaka muda wa kufanya mambo mengine ya maana unaisha halafu unajisemea nitafanya kesho na kesho ikifika yana kuwa ni yale yale tu. Tabia sugu inaweza kuwa ni uvutaji sigara unajitahidi 

lakini bado unashindwa kuacha kuvuta sigara.  Inaweza kuwa ni ulevi, unajitahidi uache kunywa pombe lakini unashangaa  umerudia kunywa pombe na unalewa vile vile, japo unapoteza fedha nyingi  ambazo ungezitumia kwenye shughuli nyingine za maendeleo. Inaweza kuwa ni uzinzi, unajitahidi uache lakini unajikuta huwezi kuacha, unaendelea kujilaumu na kujichukia lakini bado tu unafanya, hata hujui utatokaje. Inaweza kuwa ni kuangalia picha za ngono, unajitahidi uache lakini huwezi, ukibaki peke yako tu chumbani na simu au computa yako tayari unahamasika kuangalia picha za ngono na huwezi kujizuia. Tabia sugu inaweza kuwa ni kutotii ratiba yako uliyojipangia, kila mara unajitahidi uamke saa fulani ufanye kazi hii na hii lakini bado unashindwa kufanya hivyo. Hizo ni baadhi tu ya tabia sugu kwa kuzitaja. Wewe mwenyewe unajua tabia sugu yako ni ipi ambayo imekuwa inakusumbua siku nyingi na huipendi lakini ndo hivyo imekunasa.

Katika makala hii; KukiombaMsamaha Kila Kiungo Cha Mwili Wako Ni Siri Ya Ajabu Kukutoa Kwenye Tabia Sugu (kama hujaisoma naomba uisome itakusaidia), nilielezea mambo makubwa mawili yanayoharibu nafsi ambayo ni uzinzi na maneno. Lakini pia nilielezea uhusiano kati ya mwili, nafsi na wewe (maana wewe sio mwili lakini unaishi ndani ya mwili). Nikasema unapokuwa na mahusiano mabaya kati yako na mwili maana yake anayewaunganisha ili muelewane (translator) ambaye ni nafsi amejeruhiwa au amekufa kabisa. Kufa kwa nafsi maana yake imeshindwa kufanya kazi yake kisawasawa. Sasa ili nafsi yako irejee kwenye hali yake ya kawaida ni lazima kuiponya na njia mojawapo ya kuiponya nafsi ni kwa njia ya kuiomba msamaha. Baadaye nitakupa njia zingine.

Nini Kinakusumbua? Unafikiri Ni Kwa Nini?
Mahangaiko yoyote yanayokupata hasa ya moyoni chanzo chake ni kimoja tu ni kuilisha nafsi chakula kisicho sahihi. Nafsi hula chakula kupitia macho, masikio, maneno (ulimi), ngozi nk. Hivi viungo nilivyovitaja kila kimoja kwa nafasi yake na kwa wakati wake hupeleka chakula kwenye nafsi, kama chakula ni sahihi utaisikia nafsi ikifurahi, lakini kama chakula sio sahihi utaisikia nafsi ikihuzunika na kukosa amani halafu unapata mahangaiko mengi moyoni. Mambo yoyote 

yale yanayoihuzunisha nafsi maana yake yanaijeruhi au yanaiua nafsi yako. Hebu fikiria ni kitu gani ambacho kimekuwa kikikuhuzunisha au kukukosesha amani mara kwa mara?. Hebu fikiria chanzo cha kuhuzunika huko ni nini? Je, ni wewe mwenyewe kwa tabia yako sugu au chanzo chake ni nje kabisa ya wewe?. Kama chanzo cha mahangaiko yako ni nje ya mwili wako mfano umesikia ndugu yako anaugua sana, gafula unapata huzuni hiyo chanzo chake ni nje yako na ni vigumu kuyaepuka mambo hayo na wala sio lengo langu kuyazungumzia hayo kwenye makala hii. Lakini kama chanzo cha huzuni yako ni wewe kutokana na tabia yako, basi fanya mambo haya manne yatakusaidia.

Jambo la kwanza: Acha kuilisha nafsi chakula chenye sumu. Chunga macho yako yasitazame mambo usiyoyapenda vinginevyo nafsi itakula sumu. Chunga maneno unayoyatamka pia kuwa makini na maneno unayoyasikia kama uko kwenye eneo lenye maneno usiyoyapenda ondoka haraka sana. Mfano mwingine, kama unapenda kuangalia miziki ya watu wakicheza uchi hapo unaiua nafsi yako, kwahiyo huwezi kujizuia kufanya uzinzi, kama sio uzinzi basi utapiga punyeto. Kwanini itakuwa hivyo? kwa sababu nafsi inakuwa imejeruhiwa haifanyi kazi yake kawaida. Bila kuiponya nafsi uwe na uhakika hiyo itakuwa tabia sugu kwako na hutaweza kuiacha mpaka umeacha kuilisha nafsi chakula chenye sumu.

Jambo la pili; Fanya juhudi za kujipatanisha wewe na mwili wako. Njia pekee iliyodumu vizazi vingi ya kujipatanisha ni kupitia kuomba msamaha. Iombe msamaha nafsi yako, na kila kiungo cha mwili wako ulichokitumia kufanya uovu. Dhamiria kuacha uovu na tumia njia hii ya kuomba msamaha itakusaidia sana, yaombe msamaha macho yako, ulimi wako, miguu yako, mikono yako na kila kiungo ulichotumia kufanya uovu.

Jambo la tatu: Kaa mbali na marafiki wanaokurudisha nyuma. Usijidanganye kwamba nitakuwa nao tu lakini nitakuwa najiepusha na matendo yako. Kumbuka kuna msemo usemao;  “je, unaweza kuweka kaa la moto kifuani na nguo zako zisiungue?” Au “je, unaweza kukanyaga kaa la moto na nyayo zako zisiungue?”. Kuwa makini na hilo, kumbuka hata maneno unayoyasikia yanaweza kuharibu nafsi yako.

Jambo la nne: Usijaribie kufanya uovu eti kwa kisingizio kwamba sasa nimeshajua niko makini sitafanya. Hapo unajidanganya tu, lazima utafanya kama sio leo utafanya kesho kwa kisingizio hicho hicho cha kujaribia tu.

Usipoyazingatia Hayo Kuna Madhara Yoyote?
Usipoyazingatia hayo hutafanya kile unachokitaka, lazima utafanya usiyoyataka halafu utaendelea kuumia moyoni mwako siku zote. Kama una kazi ya kutumia akili, ufanisi wako kwenye kazi hiyo utakuwa mdogo kwa sababu ya kuhuzunika na kujuta. Ni vema ukayazingatia ikiwa unataka kuishi maisha mazuri yenye furaha na amani na mafanikio.

Ushauri Wa Mwisho Kwenye Swala Hili.
Soma kitabu hiki The mastery of loveKitakusaidia kushinda kila tabia sugu inayokusumbua. Nakutakia utekelezaji mwema na Mungu akusaidie uvuke kwenye mahangaiko hayo.

“Tabia sugu maana yake ni mwenendo na matendo ambayo umekuwa ukiyafanya, lakini hupendi uyafanye kwa sababu yanakuharibia maisha yako, tena yanakupotezea muda, kibaya zaidi yanakurudisha nyuma kwenye harakati zako za kuelekea mafanikio makubwa”

Tunakuhamasisha Ili Ufikie Mafanikio Yako
Share:
Top Servicare. Powered by Blogger.

Web Design

Popular Posts

INSTAGRAM FEED

@soratemplates

Blog Archive

About