Wednesday, November 4, 2015

NAMNA YA KUPATA KIBALI CHA UJENZI WA NYUMBA ILI USIJE UKAPIGWA STOP WAKATI WA UJENZI WA NYUMBA YAKO



Kutokana na kuongezeka kwa ujenzi holela sehemu za mijini, Serikali iliamua kuandaa sheria ya mipango miji inaitwa “Sheria ya Mipango Miji namba 8 ya mwaka 2007”. Sheria hiyo inaelekeza namna ya upangaji wa miji.  Moja ya maagizo ya sheria hiyo inamtaka kila mtu anayejenga nyumba kwenye eneo liliotangazwa kuwa eneo la mipango miji awe na kibali cha ujenzi na asipokuwa na kibali hicho hatua zaidi huchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa kujenga.
Kwa kufuata maagizo ya sheria hiyo kila halmashauri nchini huandaa sheria ndogo ndogo (by laws) za namna ya utoaji wa kibali hicho cha ujenzi. Sheria hizi ndogo ndogo  hutofautiana kutoka halmashauri moja hadi nyingine. Lakini angalau huwa kuna mlolongo unaokaribiana katika utoaji kibali hicho. Nachukua nafasi hii kukushrikisha mlolongo (hatua) za kupata kibali hicho.

Hatua ya kwanza: Andaa Ramani Ya Nyumba Utakayoijenga
Unatakiwa kuwa na ramani ya nyumba utakayo ijenga. Ramani unaweza kuipata kwa mtu yeyote anayechora ramani za nyumba mfano anaweza kuwa Msanifu ramani, au Msanifu Majengo anaweza kukuchorea ramani nzuri.



Hatua Ya Pili: Ramani Hiyo Inatakiwa Kuidhinishwa Na Msanifu Majengo (Architect) Aliyesajiliwa.
Lengo la Msanifu Majengo kuiidhinisha ramani hiyo ni ili kuangalia ubora na vigezo muhimu vinavyotakiwa kwenye nyumba. Pia likitokea tatizo kwenye nyumba hiyo Archtect atawajibika kujibu ikiwa tatizo hilo litatokana na kosa la mchoro wa nyumba hiyo. Wasanifu majengo waliosajiriwa wako wengi kwenye kila mkoa. Ulizia tu utawapata, kinachotakiwa Msanifu majengo huyo atapiga mhuri wake aliopewa na Bodi ya usajiri wa wasanifu majengo kwenye kila ukurasa wa ramani hiyo.
Huwa kuna gharama kidogo kwenye kuidhinisha ramani kwa architect kulingana na aina ya ramani, mfano kama ni ramani ya nyumba ya kuishi yenye vyumba vitatu au vine kuna wengine huwa wanafanya shilingi 50,000/= na wakati mwingine huwa zaidi ya hapo.

Hatua Ya Tatu: Chukua Fomu Kutoka Ofisi Ya Ujenzi Na Uzipitishe Zisainiwe Kila Sehemu Inayohitajika
Fomu hizi zinatakiwa zipitishwe kwa Afisa Ardhi wa Wilaya husika, kwa Afisa Mipango Miji na kwa Bwana Afya wa Wilaya. Sehemu hizo zote kila mmoja atakagua mambo yake. mfano, Afisa Ardhi atakagua kama kiwanja kinamilikiwa kihalali na kinalipiwa kodi ndio maana unatakiwa uambatanishe na Hati au Offer ya kumiliki kiwanja na risiti ya malipo ya kodi ya kiwanja ya hivi karibuni.

Afisa Mipango Miji atakagua aina ya nyumba unayotaka kujenga na matumizi yake na atalinganisha kwenye ramani ya mipango miji ajue eneo unalotaka kujenga hiyo nyumba linepangiwa matumizi gani. Kama eneo unalotaka kujenga limetengwa kwa ajili ya viwanda na wewe unataka kujenga nyumba ya makazi hata kubali kusaini kwenye sehemu yake. Bwana Afya atakagua ukubwa wa madirisha na uhusiano wa matumizi ya chumba kimoja na kingine. Pia atakagua shimo la maji taka (septic tank). Ukimaliza kupitisha huko utairudisha fomu hiyo ofisi ya ujenzi.

Hatua Ya Nne: Kutembelea Kiwanja Na Kujiridhisha.
Baada ya hapo Mhandisi wa Ujenzi itabidi uende naye kwenye kiwanja unachotaka kujenga ili akajaze taarifa za kiwanja chako na akajiridhishe kama kiwanja kweli kipo. Taarifa ya kiwanja chako atazijaza kwenye fomu hizo kuna sehemu ya kujaza Mhandisi wa Ujenzi. Halafu atapiga mhuri wa ofisi ya ujenzi kama ishara ya kwamba kila kitu kiko vizuri.

Hatua Ya Tano: Kuidhinishwa Na Kamati Ya Ujenzi Ya Wilaya Husika.
Mhandisi wa ujenzi akisha kagua kiwanja chako na akajaza taarifa zake kwenye fomu, kinachofuata ramani hiyo na fomu zote itapelekwa kwenye kikao cha kamati ya ujenzi ya Wilaya ambacho hukaa mara moja kila baada ya muda fulani mfano kuna baadhi ya halmashauri kamati hiyo hufanya kikao chake kila baada ya miezi mitatu. Kikao hicho ndicho kitaidhinisha kutolewa kwa kibali cha ujenzi wa nyumba unayotaka kujenga.

Hatua Ya Sita: Kibali Kinatolewa.
Mara baada ya kikao cha kamati ya ujenzi kumalizika, vibali vyote vilivyoidhinishwa kutolewa, hutolewa kwa wahusika. Kinachotakiwa wakati wa mchakato wote huo uwe na nakala 3 au 4 za ramani yako ya nyumba ili mara baada ya kutolewa kwa kibali cha ujenzi nakala moja atabaki nayo mwenye nyumba, nakala nyingine itapelekwa Ofisi ya Ardhi ya wilaya na nakala moja itabaki kwenye Ofisi ya Ujenzi kama kumbukumbu.
Ukipata kibali chako unaweza kuendelea na ujenzi wako kwa amani bila bughuza. Kutokuwa na kibali cha ujenzi ukibainika unaweza kuzuiliwa kujenga (stop order) mpaka utakapopata kibali cha ujenzi.


“Moja ya maagizo ya sheria hiyo inamtaka kila mtu anayejenga nyumba kwenye eneo liliotangazwa kuwa eneo la mipango miji awe na kibali cha ujenzi na asipokuwa na kibali hicho hatua zaidi huchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa kujenga

Tunakutakia kila la heri katika ujenzi wa Taifa. TOPSERVICECARE
Share:

0 comments:

Post a Comment

Top Servicare. Powered by Blogger.

Web Design

Popular Posts

INSTAGRAM FEED

@soratemplates

Blog Archive

About