Saturday, October 31, 2015

UFAHAMU WAKATI MZURI WA KUPATA MAWAZO MAPYA NA KUJIONA MWENYEWE

Habari Ndugu:
Katika maisha yako umesha chunguza na ukafahamu ni wakati gani huwa unapata mawazo mapya au ni wakati gani huwa unajisikia furaha utulivu wa akili na hatimaye unapata nguvu mpya ya kusonga mbele kwenye maisha yako? Je, ni wakati ukiwa umelala?, ni wakati ukiwa unaangalia mpira?, ni wakati ukiwa na rafiki yako? Ni wakati ukiwa baa? Au ni wakati gani?
Dunia imejaa kelele nyingi kila mahali, kuna kelele za magari, kuna kelele za watu, kuna kelele za mihemko ya mwili na kuna kelele za wanyama na ndege 

wa angani. Tunayo bahati kubwa sana miili yetu inauwezo wa kuchuja hizo kelele na hatimaye hazikuathiri sana lakini katikati ya kelele hizo  ni vigumu sana kupata wazo jipya na kujiona mwenyewe. Pia katikati ya kelele hizo ni vigumu sana kupata nguvu mpya.
Kuna rafiki yangu mmoja nilimwuliza hivi;  “Ni wakati gani huwa unapata mawazo mapya?” “Akasema kwa kweli mara nyingi sana nikiwa naangalia mpira huwa napata mawazo mapya na siku nyingine nikiwa napiga stori na marafiki zangu huwa napata mawazo mapya”.
Nikamwuliza kwa namna hii “Ni wakati gani huwa unajiona mwenyewe? Akashangaa! kujiona mwenyewe? Mbona kila siku huwa najiona hata sasa najiona au unamaanisha nini? Nikamwambia sina maana nyingine ni hiyo hiyo ni wakati gani huwa unajiona mwenyewe? Akasema hapo sijakuelewa naomba ufafanuzi.


Nikaanza kumweleza; mara nyingi sana sisi binadamu huwa hatujioni sisi mwenyewe lakini huwa tunawaona watu wengine, pale wanapofanya mambo mazuri wakati mwingine huwa wa kwanza kutoa maoni yetu juu ya mafanikio hayo au wanapofanya vibaya huwa vile vile wa kwanza kutoa maoni yetu juu ya kufanya vibaya kwao. Wakati tunatoa maoni yetu juu ya watu wengine macho yetu na akili zetu huwa zinasahau kujiona (kujiangalia) sisi wenyewe. Kwahiyo kujiona wewe mwenyewe (finding yourself) ni kule kujitambua kutoka ndani 

yako sehemu ulipo katika mambo yote, mfano kiuchumi, kiroho, kielimu n.k
Mtu anayejiona yeye mwenyewe anakuwa makini na anakuwa na kiu ya kutaka afike sehemu fulani, hapotezi muda bure kwenye mambo yasiyomsaidia kwenye maisha yake, tena mtu anayejiona yeye mwenyewe sio mwepesi wa kutoa maoni juu ya watu wengine maana kabla hajatoa maoni juu ya watu wengine jicho lake litamwona yeye kwanza. Baada ya maelezo hayo akasema hapo nimekuelewa.
Ninachotaka nikushirikishe ndugu kwenye makala hii ni kwamba  kuna wakati ambapo mtu anaweza kujiona yeye mwenyewe wakati huu anapojiona yeye mwenyewe ndipo anapata mawazo mapya yenye kumjenga. Je, ni wakati gani huo?


Ni wakati wa KUPUNGA. Kupunga ndio nini? Kupunga ni wakati ambapo mtu anaenda sehemu tulivu yenye mandhari nzuri na mara nyingi wakati wa jioni au mchana kwa lengo la kutafakari. Mtu huenda kwenye eneo hilo akiwa peke yake. Kupunga ni namna ya kupata mawazo mapya na kujiona wewe mwenyewe na njia hii ilitumiwa tangu enzi za mababu wa kale na kale. Walikuwa wanatumia njia hii ya kupunga kondeni hasa mara baada ya kazi ngumu. Baadaye katika kizazi chetu watu wameanzisha utaratibu wa kwenda 

kupunga na marafiki zao sehemu za fukwe ya bahari au ziwa.
Lakini kupunga yenye lengo la kupata mawazo mapya na kujiona wewe mwenyewe unatakiwa uwe peke yako ukitafakari jinsi ulivyo, maisha yako yalivyo, mwelekeo wako utakuwaje lakini pia ukifurahia mandhari nzuri ya uso wa dunia na wakati mwingine miziki ya sauti za ndege ikiimba kwa mbali. Wafalme wengi walitumia njia hii ya kupunga ili kupata utulivu wa akili na utulivu wa moyo katika kutawala kwao na  jinsi ya kukabiliana na maadui zao.

Je, wewe huwa unapunga?. Kuna faida nyingi sana za kupunga, mimi baada ya kuzifahamu faida hizo mara nyingi huwa napunga. Utanikuta niko sehemu tulivu yenye mandhari nzuri au wakati mwingine huwa naenda mlimani napanda juu ya mlima halafu naanza kufurahia jinsi dunia ilivyo nzuri, jinsi mimi mwenyewe nilivyo mzuri, si hayo tu bali huwa napata msimamo wa maisha yangu. Toka nikiwa kidato cha kwanza nilianza tabia hii ya kupunga mpaka sasa naendelea, kwa kweli ni furaha kubwa. Naomba nikushirikishe baadhi ya faida unazozipata kwa kupunga.

Kubadili msimamo hasi wa kimawazo.
Kupitia kupunga huwa nabadilika kabisa jinsi ya kufikiri kwangu, wakati mwingine huwa moyoni nimejaa fikira potofu za mahangaiko ya hapa na pale lakini nikienda kupunga nguvu mpya hunijia na  mawazo mapya ya kukabiliana na changamoto za maisha yaninijia.

Kupata furaha na raha ya kuishi duniani.
Ni kweli kabisa kama nilivyokudokeza hapo mwanzo, wafalme wengi na mpaka hivi sasa utakuta wana bustani kubwa na nzuri mara nyingi saa za jioni huenda 

kwenye bustani zao na kufurahia maisha. Mara nyingi mimi nikiwa napunga huwa nafurahi sana kuona mimi ni mzima mwenye afya na huwa nafurahi sana kuona dunia jinsi ilivyo nzuri. Zaidi ya yote huwa nafurahi sana ninapowasikia na kuowaona ndege jinsi wanavyoimba na kufurahi. Nikiwa napungia ufukweni huwa nafurahi sana kuona jinsi bahari au ziwa linavyopendeza na wakati mwingine nikiwaona viumbe vya bahari wanavyofurahia maisha wakiruka ruka kwenye ulimwengu wao.

Kutoa wivu, hasira na kujaa upendo.
Wakati mwingine huwa tunakwazwa na mambo mengi sana katika maisha. Ukiwa na tabia ya kupunga utashangaa hizo sumu zinatoweka na badala ya kuwa na hizo sumu unakuwa na upendo mwingi. Kwanza unajipenda wewe mwenyewe na unajiona ni mwenye bahati. Lakini pia kama utakuwa unapungia eneo lenye ndege au wanyama, viumbe hao watakufundisha jinsi wanavyoishi kwa kupendana wakifurahi siku zote.

Kujiona wewe mwenyewe.
Hili ndilo lengo hasa la makala hii, wakati wa kupunga ni wakati wa kujiona wewe mwenyewe. Ndio maana nakushauri unapopunga kwa lengo la kujiona wewe mwenyewe unatakiwa uwe peke yako. Wakati ukiwa unatafakari tafakari utashangaa utakapojiona wewe mwenyewe jinsi ulivyo mzuri, ulivyo barikiwa, tena utajiona wewe mwenyewe jinsi unavyotakiwa kuongeza juhudi kwenye mambo yako mazuri nk. Unapokuwa kwenye kelele nyingi sio rahisi kujiona wewe mwenyewe wala hutajigundua jinsi ulivyo. Nakushauri kama unanafasi anza tabia hii ya kupunga utashangaa jinsi utakavyojiona wewe mwenyewe.

Unapokuwa unapunga ufanye nini zaidi?
Unapopunga unatakiwa kuwa kwenye eneo lenye utulivu, ni vizuri ukazima simu yako ili ubaki peke yako. Unapopunga jifurahie wewe mwenyewe, pumua kwa nguvu halafu jisikilizie jinsi ilivyo raha kupumua, utashangaa wakati unapumua kwa namna hii utaona kila kitu kinachokuzunguka jinsi kilivyo kizuri, anga litakuwa zuri miali ya mwanga itakuwa inadunda dunda hata hakuna lugha ya kuielezea.

Ushauri wangu.
Mpendwa msomaji wa Top Service Care nakushauri anza kuwa na tabia ya kupunga angalau tenga hata siku moja kwa wiki saa ya jioni mara baada ya kazi nenda kwenye eneo zuri ukapunge. Kunafaida kubwa sana ya kupunga hata Mungu mwenyewe huwa anapunga saa ya jioni kama ilivyoandikwa kwenye 

kitabu cha Mwanzo. Mimi naamini nguvu iliyomo wakati wa kupunga, na nitaendelea siku zote kupunga nipatapo nafasi. Kama hujaanza wala hujawahi kujaribu basi mara umalizapo kusoma makala hii jiwekee ratiba ya kupunga halafu utaniambia jinsi ilivyo raha kupunga. Unaweza kuniandikia kwa email
“Kupunga ni namna ya kupata mawazo mapya na kujiona wewe mwenyewe na njia hii ilitumiwa tangu enzi za mababu wa kale na kale. Walikuwa wanatumia njia hii ya kupunga kondeni hasa mara baada ya kazi ngumu”

Tunakuhamasisha ili ufikie mafanikio yako
Share:

0 comments:

Post a Comment

Top Servicare. Powered by Blogger.

Web Design

Popular Posts

INSTAGRAM FEED

@soratemplates

Blog Archive

About