Saturday, October 31, 2015

UTAMU WA MAISHA HUU HAPA

Furaha niliyonayo, haina tena mfano,
Nacheka napiga mwayo, na kuubusu mkono,
Umeburudika moyo, kwa usingizi wa pono,
Njoo mwaka kesho njoo, nende zangu sekondari.

Ndugu nimeanza kwa kionjo cha shairi hilo nikitaka tujifunze kitu. Shairi hilo nalikumbuka lilikuwa limeandikwa kwenye kitabu cha Jipime Kiswahili,shule ya msingi. Kabla ya shule za kata kuanzishwa, kufaulu kutoka shule ya msingi kwenda sekondari ilikuwa kitu kigumu sana hasa kwa wale waliokuwa wanaishi vijijini. Ilikuwa raha kubwa ikitokea ukafaulu na kuwa miongoni wa wanafunzi wachache walioweza  kwenda sekondari. Sasa, tunajifunza nini kwenye shairi hili?. Kama kichwa cha habari hapo juu ilikuwa inaonekana kwamba ukifaulu kujiunga na masomo ya sekondari, huko sekondari maisha ni matamu sana. Lakini mara nyingi ilikuwa tofauti, ilikuwa ukifika sekondari enzi zile unanyanyaswa halafu unaonekana hufai katika dunia hii. Utamu wa maisha uliokuwa unauwazia unakuwa kinyume chake. Kumbe maisha matamu haikuwa kwenda sekondari.

Naomba nikuletee hadithi tatu kuhusu utamu wa maisha kisha kupitia hadithi hizo tatu tutapata kufahamu maisha matamu ni yapi.

Hadithi ya kwanza: Utamu wa maisha ni kupata watu wengi wanaokuunga mkono au kukushangilia. Kuna mtu mmoja alikuwa mchezaji wa mpira wa miguu, kwa sababu alikuwa anafanya vizuri sana kwenye mchezo huu, watu wengi walikuwa wanamshabikia. Baada ya kuwa mchezaji bora kwa muda mrefu, mtu mmoja akamwuliza hivi utamu wa maisha ni nini? Yule jamaa akajibu haraka haraka akasema "Utamu wa maisha ni pale watu wengi wanapokuunga mkono kwenye kazi zako". Muda sio mrefu yule  jamaa akavujika mguu wakati anacheza mpira, cha kushangaza wale waliokuwa wanamshabikia hawakumshabikia tena. Kibaya zaidi hata kule kumfariji tu hawakuja. Baada ya kuona vile akabadilisha mawazo yake akaanza kusema jamani utamu wa maisha sio kuungwa mkono na watu. Tangu siku hiyo akaanza kuwaambia watu wote hata watoto wake kwamba maisha matamu sio kupata washabiki wengi kwa sababu ipo siku hao watu wanaookuunga mkono watakuacha. Kwahiyo maisha matamu sio kuungwa mkono au kushabikiwa na watu.

Hadithi ya pili: Maisha matamu ni kuoa au kuolewa. Kuna mtu mmoja wanaume, kwa muda mrefu alikuwa akiulizwa maisha matamu ni yapi? Alikuwa anatoa jibu moja tu “ Maisha matamu ni pale unapokuwa na mke wako”. Tena katika mahali pale kulikuwa na mwanamke mmoja naye alikuwa akiulizwa maisha matamu ni yapi?. Alikuwa anatoa jibu moja tu “maisha matamu ni pale unapokuwa na mume wako”. Siku si nyingi wale watu walioana; maisha yakaendelea, miezi kadhaa ikapita.  Kweli walikuwa wanakiri wote kuwa maisha matamu ni kuoa au kuolewa. Mwanaume alikuwa anafanya kazi kiwandani, kiwanda cha kutengeneza vitu vya urembo. Siku moja kuna  muuza sukari alipita kwenye familia ya wanandoa hao akiwa anauza sukari; akamkuta mwanamke yupo, mwanaume kama kawaida alikuwa kazini kwake. Yule muuzaji akampenda yule mwananke na akamtaka kimapenzi na kwamba akifanya nae mapenzi atampa sukari bure. Yule mama akakataa lakini baada ya kumshawishi kwa maneno mengi hatimaye akawaza si mara moja tu halafu mume wangu hatajua. Basi, akamkubalia wakaanza kufanya mapenzi.
Siku hiyo kule kiwandani walikuwa wanazindua saa mpya, mume wa yule mwanamke akasema ngoja nichukue hii nimpelekee mke wangu ili awe wa kwanza kuivaa. Akakimbia mbio kwenda nyumbani, kufumba na kufumbua akamkuta mke wake anafanya mapenzi na yule muuza sukari. Mambo yakageuka akamchukia sana  mke wake na hakutaka tena kuishi naye, japo yule mwanamke aliomba msamaha, mume wake alikataa katu katu. Mwisho wa yote yule mwanamke akasema heri nisingekuwa nimeolewa kumbe maisha matamu sio kuolewa. Baada ya maneno hayo akajinyonga hadi kufa. Baada ya kufa, yule mwanaume alikamatwa na kufungwa jela. Akiwa jela akajisemea afadhali kama nisingekuwa nimeoa. Akaendelea kusema kumbe maisha matamu sio kuoa. Kutokana na hadithi hiyo tunapata kufahamu kuwa kumbe maisha matamu sio kuoa au kuolewa.

Hadithi ya tatu: Maisha matamu ni kuwa na mali nyingi. Kuna watu wawili mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa masikini. Siku moja yule masikini akaugua sana. Yule tajiri aliposikia kwamba yule masikini anaumwa akaenda kumsalimia, akamhurumia sana kwa jinsi alivyokuwa anaumwa akawa anawaza; sasa huyu masikini ataponaje! afadhali kama angekuwa na pesa angekuwa ananunua hata matunda. Kwa kumhurumia akawa kila akienda kumsalimia anamwachia shilingi 500/=. Yule tajiri akaendelea hivyo hivyo hatimaye masikini akapona.
Siku si nyingi tajiri naye akaugua sana, akalazwa hospitali.  Yule masikini akawa anaenda kumsalimia , halafu kila akienda kumsalimia anamwachia shilingi 500/=. Pamoja nakwamba yule tajiri alikuwa na kila kitu na matunda ya kila aina, hakuweza kuyala. Baada ya hali kuwa mbaya akaanza kusema “ Jamani maisha matamu sio kuwa na mali nyingi”. Siku moja aliwaita watoto wake akaanza kuwaambia kama nitakufa waambieni watu wote kuwa maisha matamu sio kuwa na mali nyingi. Kweli muda sio mrefu  tajiri akafa akamwacha yule masikini anaishi. Kutokana na hadithi hiyo tunapata kufahamu kwamba maisha matamu sio kuwa na mali nyingi.
  
Kama Ni Hivyo, Maisha Matamu Ni Yapi Basi?
Siri ya maisha ni fumbo kubwa lakini ukikaa na kufikiri vizuri unaweza kupata picha jinsi maisha matamu yalivyo. Tumekuwa kukihangaika usiku na mchana tukitafuta maisha matamu. Mawazo ya watu wengi ni kwamba maisha matamu ni kuwa na mali nyingi, na kwa sababu hiyo watu wamekuwa wakipambana kwa kila namna ili wapate pesa au wawe matajiri, eti wakifikiri kuwa wakiwa matajiri watakuwa na maisha matamu. Lakini ukweli ni kwamba maisha matamu hayaletwi na mali.

Falsafa yangu: Maisha Ni Mchezo
Tangu nianze kuitumia falsafa hii, imenisaidia kuelewa maisha matamu ni kitu gani. Nimetumia muda mwingi kufikiri maana halisi ya maisha, utamu wake na uchungu wake. Baada ya kufikiri namna ile nilipata kufahamu kuwa maisha yote anayoishi mtu hapa duniani ni mchezo (is a game). Unacheza kwa namna mbalimbali mfano, unaweza kucheza mchezo wa kufatuta pesa, unaweza kucheza mchezo wa kusaidia watu wengine, unaweza kucheza mchezo wa mpira wa miguu, unaweza kucheza mchezo wa siasa, unaweza kucheza mchezo wa masumbwi nk.

Chukulia kwa mfano, wanandoa wanapotengeneza mtoto ni mchezo mojawapo kama ilivyo michezo mingine. Mchezo wa ngumi umenisumbua sana kichwani mwangu nilikuwa nawaza hivi inakuwaje mtu achague mchezo wa ngumi! mbona ni mateso makubwa?. Baadaye nimekuja kufahamu kuwa, mchezo huu ni sehemu ya maisha kwahiyo hakuna mchezaji anayecheza mchezo amechukia. Kama utacheza mchezo wowote ukiwa huna furaha unapocheza lazima utashindwa mchezo huo. Kama unafikiri nadanganya waulize wachezaji wanaokimbia mbio ndefu au fupi wote wanacheza kwa furaha kubwa japo kama hujawahi kimbia kama mchezaji;  siku ukikimbia utakiona cha mtema kuni ni mateso makubwa. Lakini kwa mchezaji ni raha kubwa.

Baada ya kuanza kuitumia falsafa hii imekuwa msaada mkubwa sana kwenye maisha yangu. Mfano nikiwa  nalima shambani naweza kulima  toka asubuhi mpaka jioni bila kuchoka kwa sababu silimi kama mkulima nalima kama mchezaji. Nachukulia kulima kama mchezo mmojawapo kati ya michezo mingine. Nikiwa ofisini nachukulia kuwa ofisini kama mchezo, kama ilivyo michezo mingine hata kama atakuja mtu wa kumhudumia nafurahi zaidi kwa sababu nacheza mchezo ninaoupenda.

Chukulia Kwa Mfano Siasa
Siasa ni mchezo kama ilivyo michezo mingine. Ndio maana utawakuta wanasiasa wanabadilishana vyama leo alikuwa chama hiki kesho anahamia chama hiki. Wewe ambaye sio mchezaji utaona kama kitu kigeni kwa sababu wewe sio mchezaji na hujui sheria za mchezo huo. Ni kama vile mchezaji wa Yanga anavyoweza kuhamia Simba na akaendelea kubaki kuwa mchezaji. Kama kwenye timu za mpira wa miguu mchezajia anaweza kuhamia timu nyingine pinzani na akahesabika yuko sahihi, kwanini unashangaa ukiwaona wanasiasa wanahamia vyama vingine?. Siasa ni mchezo kama ilivyo michezo mingine. Kuongoza watu ni mchezo kama ilivyo michezo mingine. Viongozi wote tulionao wanacheza kila mmoja na nafasi yake, kama vile kwenye mchezo wa mpira wa miguu kila mtu anachezea namba yake. Vivyo hivyo viongozi wetu wanacheza kila mtu na namba yake uwanjani ila mchezo ni mmoja tu “Uongozi

Nataka Kuwa Tajiri
Napenda kutafuta pesa, napenda kuwekeza, napenda kuanzisha miradi mingi niwezavyo, nafanya hivyo kwa sababu huo ni aina ya mchezo ninaoupenda kuucheza. Sitafuti pesa kama natafuta maisha natafuta pesa kwa kucheza mchezo wa kutengeneza pesa. Nafurahi zaidi nikiwa nacheza mchezo huu, sipendi kucheza peke yangu napenda kucheza kama timu kwa sababu nafahamu ili nishinde mchezo wowote lazima nishirikiane na watu wengine wanaocheza nami ndio maana nakushirikisha wewe ndugu kwenye mchezo huu. Nakuandikia makala hizi ili zikutie moyo halafu uwe mchezaji mzuri. Nafahamu kwenye mchezo wowote kuna kushinda , kushindwa au kutoka sare. Siku nikipata hasara kwenye miradi yangu nafurahi zaidi kwa sababu ni sehemu ya mchezo, lakini siishii kufurahi tu nachukulia kitu kilichonifanya nipate hasara kama somo. Siumii sana moyoni nipatapo hasara najua ili nishinde mchezo huu lazima nikutane na changamoto hizo ili ziniimarishe. Napenda utajiri, wala sifikirii kuwa tajiri ndio nitakuwa na maisha matamu. Kuwa tajiri kwangu ni fursa mojawapo itakayoniongezea wigo wa kucheza michezo mingi zaidi katika maisha yangu, pia utajiri utanisaidia kuwa na wigo mpana zaidi wa kuwasaidia watu wengine kwenye michezo yao ili nao wazidi kufurahi zaidi.

Mungu Ni Mchezaji Mzuri
Ndiyo, Mungu anapenda sifa, anapenda watu wamwimbie anapenda watu wacheze, ndio maana katika maandiko matakatifu anatushauri tumwimbie na kumchezea, anapenda sana michezo lakini anasema tusicheze bila yeye lasivyo michezo yetu itageuka kuwa taabu badala ya kuwa mchezo.

Ona anavyosema: “Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao Mungu watapata nguvu mpya, watapanda juu kwa mbawa kama tai, watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu , wala hawatazimia. Isaya 40:30-31”

“Msifuni kwa matari na kucheza; msifuni kwa zeze na filimbi. Kila mwenye pumzi na amsifu Mungu. Zaburi 150:4-6”

Nimekupa mifano hiyo miwili ya maandiko matakatifu kuonyesha Mungu anapenda watu wake tucheze. Unaweza kutafuta maandiko mengine mengi zaidi kwenye dini yako. Mungu anafurahia kuona dunia inalizunguka jua, mwezi unaizunguka dunia na mambo mengine mengi, yote hayo ni michezo aliyoianzisha yeye ili imfurahishe. Maisha yote ni michezo mbalimbali ambayo kwa pamoja inatengeneza kitu kinachoitwamaisha.


Maisha Matamu Nimepata Jibu Lake
Baada ya kuanza kuitumia falsafa hii, kwamba maisha ni mchezo, imeniongezea zaidi wigo wa kufikiri. Lakini katika yote nimeelewa kuwa maisha matamu ni kuwa hai,kuwa mzima wa afya na kufurahia kucheza pamoja na Mungu. Haijalishi unapesa au huna, maisha ni mchezo. Kama unaona maisha ni mateso au ni magumu ni kwa sababu hupendi kucheza mchezo huo, unataka ufanye nini sasa?

Ushauri Wangu Kwako
Kwa sababu maisha yote ni mchezo, unatakiwa ujifunze tabia za michezo mbalimbali. Anza kujifunza kucheza, na siku zote hakuna mchezo unaocheza huku huupendi, kama utacheza mchezo ukiwa umekasirika au unamawazo lazima utafanya vibaya kwenye mchezo huo. Ukiwa kwenye ndoa, ndoa ni mchezo cheza kama mchezaji, ukiwa masomoni, masomo ni mchezo soma kama mchezaji. Kuna michezo mingine inasheria zimeandikwa kama mpira wa miguu lakini kuna michezo mingine sheria zake hazijaandikwa ni lazima uzitafute kwa kusoma vitabu mbalimbali au kuhudhuria semina. Mchezo wa kutafuta pesa ni miongoni mwa michezo ambayo sheria zake utazipata kwa kusoma vitabu na  kujifunza. Anza kufurahia maisha sasa. Usifikiri kwamba, kazi unayoifanya ni ngumu, kama unafikiri ni ngumu hebu fikiria kuhusu mchezo wa mgumi,  je, ni mchezo rahisi? Kama sio rahisi mbona kuna watu wanapenda kucheza?. Jibu ni rahisi tu maisha yote ni mchezo, cheza kwa furaha huku ukifurahia utamu wa maisha yako ukiwa unacheza.
Lakini kumbuka ili ushinde mchezo wowote lazima utii sheria zake, vinginevyo hutashinda kamwe.

“Tumekuwa kukihangaika usiku na mchana tukitafuta maisha matamu. Mawazo ya watu wengi ni kwamba maisha matamu ni kuwa na mali nyingi, na kwa sababu hiyo watu wamekuwa wakipambana kwa kila namna ili wapate pesa au wawe matajiri, eti wakifikiri kuwa wakiwa matajiri watakuwa na maisha matamu. Lakini ukweli ni kwamba maisha matamu hayaletwi na mali”.

Tunakuhamasisha ili ufikie mafanikio yako

Share:

0 comments:

Post a Comment

Top Servicare. Powered by Blogger.

Web Design

Popular Posts

INSTAGRAM FEED

@soratemplates

Blog Archive

About