Saturday, October 31, 2015

HATUA ZA KUCHUKUA PALE NDUGU ZAKO WAKARIBU WANAPOKUCHUKIA

Ndugu nakusalimu!
Mwanzoni mwa mwezi huu wa Oktoba, nimekutana na rafiki yangu mmoja, anaishi na mke wake na wanamtoto mmoja. Mwaka mmoja uliopita alifiwa na wazazi wake wote hivyo akabaki yeye na mke wake kwenye familia hiyo, na akateuliwa na wanandugu awe msimamizi mkuu wa mali za wazazi wake yakiwemo mashamba na mali nyingine. Mara baada ya kupewa jukumu hilo, 

kuna baadhi ya wanandugu hawakufurahishwa na madaraka aliyopewa ikizingatiwa kwamba yeye ni mdogo kuliko wote, anaumri wa miaka 26. Matokeo ya kupewa madaraka hayo yamewafanya baadhi ya wanandugu wamchukie,  hata kufika hapo nyumbani hawafiki au wakija wanaishia kwa majirani huku wakimsema kwa kila neno baya. Ingekuwa heri kama wangeishia 

kumsema kwa maneno tu lakini kuna wengine wanaenda mbali zaidi kwa kumtafutia dawa za kumloga ili wamharibie kabisa mambo yake.
Jumapili iliyopita ya 04/10/2015 nilimtembelea nyumbani kwake, nimemkuta anahali mbaya kimawazo huku hajui afanye nini. Kibaya zaidi yeye na mke wake hawanamatumaini ya kusonga mbele kiuchumi.

Je, Wewe unahali Kama Hiyo Au Inafanana Na Hiyo?
Huenda wewe ndugu umekumbana na mkasa wa namna hiyo wa ndugu kukuchukia kwa sababu mbalimbali. Wanaweza kuwa ni ndugu zako wa ukoo au wanafunzi wenzako au wafanyakazi wenzako au jamaa zako wa karibu wanakuchukia,  hata ukisema chochote hawakuelewi zaidi ni kukutukana au kukunenea mabaya. Anaweza kuwa ni mtu mmoja anakuchukia na anakutesa kwa mateso mengi kiasi kwamba unashindwa namna ya kufanya. Wakati mwingine umekuwa na wasi wasi na maisha yako. Je, katika mazingira kama hayo utafanya nini?

Fanya Mambo Haya Kuvuka Mahali Hapo.

Jambo la kwanza: Hakuna mtu badala yako, pambana kwa ajili ya maisha yako. Fahamu kuwa hakuna mtu yeyote duniani atakayebeba maisha yako. Mtu anayekuchukia na kukufanyia mambo mabaya analengo la kukuchelewesha kwenye safari yako ya mafanikio. Kama utaendelea kujibizana naye au kumnunia unachelewa kwenye mafanikio, halafu unapoteza njia yako. Unachotakiwa kufanya ni kusonga mbele usikubali maneno ya mtu yakujeruhi moyoni mwako nakukutoa kwenye mstari wa mafanikio. Endelea na juhudi zako 

za kutafuta mafanikio waache waseme waache waongee kila neno wanalojua, wewe usiwajibu kaa kimya halafu usiruhusu neno lolote likuumize moyoni mwako. Kila unaposikia neno au matusi achana nayo wewe jifanye ujasikia songa mbele. Kumbuka adui anambinu nyingi  za kukuharibia maisha yako usimpe nafasi akuharibu kwa maneno yake. Ukianza kujibizana naye  unawasha moto wa hasira kiasi kwamba hutaweza kufanya mambo yako ya msingi.  Kwahiyo jifunze kukaa kimya na kupotezea kila neno kisha songa mbele kuelekea mafanikio yako.(Fight for your own life)

Jambo la pili: Tumia maneno mabaya kama kichocheo cha kufanikiwa zaidi. Hii ni mbinu nzuri sana ya kushinda hila na mbinu za adui wa mafanikio. Ukisikia neno baya likinenwa juu yako, usichukie furahi zaidi halafu yageuze maneno hayo yawe hamasa ya kufanya bidii zaidi kwenye mafanikio yako. Ili kuitumia mbinu hii vizuri, unatakiwa uandae taswira yako ya mafanikio ambayo mara 

kwa mara utakuwa unaiangalia na kupata nguvu ya kuifuta hadi uipate. Kwahiyo kila mtu anapokutukana humwangalii aliyekutukana unaangalia ile taswira ya mafanikio yako, kwahiyo hayo maneno aliyokutukana yanakutia uchungu wa kuifuata taswira hiyo. Fanya hivyo kwa furaha huku ukitiwa nguvu na maneno ya wanaokuchukia. Ili kuipata taswira ya mafanikio yako andaa malengo yako.

Jambo la tatu: Watu wote ni wagonjwa wa akili, kwahiyo jifunze kufurahi na kupenda kila wakati. Don Miguel Ruiz anasema watu wote hapa duniani wanamajeraha akilini mwao, kwahiyo kila mara utawakuta wanawaka hasira na kuumia moyoni mwao halafu wanatafuta mahali pa kupumzisha machungu ya kuumwa kwao. Akikupata mtu kama wewe atakuchukia na kukulaumu kwa kila jambo. Usishangae,  kwa sababu anaumwa ugonjwa wa akili. Tatizo na wewe unaumwa ugonjwa wa akili ndio maana akikutukana unachukia na kuumia moyoni mwako kwa sababu amegusa jeraha lililoko akilini mwako. Ili kushinda maumivu ya kuguswa kwa majeraha yako akilini, unatakiwa ujifunze kuwapenda watu wote hata maadui zako. Jifunze kufurahi kila mara kila neno unalolisikia ligeuze liwe furaha halafu mpende anayekunenea mabaya. Ukiweza kuitumia mbinu hii, ugonjwa wa akili yako utapona haraka halafu kila neno na chuki na lawama zitakazoletwa kwako hazitakuumiza hata kidogo badala yake utajaa upendo na furaha katikati ya chuki za wanadamu.

Jambo la nne: Kila mtu atakufa. Hii ni mbinu nyingine nzuri ya kutumia kushinda chuki na lawama za wanadamu. Kama kuna mtu atakuja kwako akaanza kukunenea kila neno baya na matusi na chuki juu yako, unatakiwa umshangae halafu waza moyoni mwako hakuna atakayeishi milele. Ukiwa makini na mbinu hii moyoni mwako, utajaa furaha kila wakati hata wakati mtu anapokuchukia na kukununia bado utakuwa na furaha na utaanza kumhurumia kwa maneno yake yasiyo na maana. Don Miguel Ruiz katika kitabu chake The Four Agreement anatuhimiza tujifunze kutoka kwa malaika wa kifo. Malaika wa kifo anatufundisha kuishi maisha ya furaha na utakatifu kila siku na kujiweka tayari kwa maana muda wowote tunaweza kufa. Tumia mbinu hii kumpuuzia kila mtu anayekulaani huku ukijua hataishi milele.

Jambo la tano: Angalia Fursa Nyingine. Kama kuna uwezekano wa kukaa mbali na watu wanaokuchukia, basi fanya hivyo. Mfano, mtu anaweza kuwa anakuchukia kwa sababu anakuona kama mzigo kwa kuwa unaishi nyumbani wake. Ukiona sababu ya kukuchukia ni hiyo, jaribu kuangalia uwezekano wa kuondoka mahali hapo. Tafuta chumba chako uanze maisha yako utajifunza mengi na mbinu za kupata pesa utazipata nyingi. Wakati mwingine sio lazima uondoke nyumbani unaweza kutafuta biashara yoyote ili uwe unaingiza pesa kidogo kidogo kuliko kukaa bure tu.

Jambo la sita:  Andaa kitengo maalum kwa ajili ya mtu anayekuchukia. Tunaona katika ulinzi na usalama wa nchi yetu, kama kuna eneo lina migogoro mingi sana ya uvunjifu wa amani, jeshi la polisi huwa linaandaa kanda maalumu kwa ajili ya kusogeza huduma karibu kwenye eneo hilo na kutatua migogoro iliyopo. Fanya vivyo hivyo kwa mtu anayekuchukia mwandalie kitengo maalumu ili usogeze huduma karibu yake zaidi kiasi kwamba ataondoa chuki yake na kukuona wa thamani kwake. Kwenye kuandaa kitengo maalumu  unatakiwa umpende na umpatie mahitaji yoyote unayoweza kumpa. Unaweza kuwandalia zawadi au unaweza kumfanyia jambo lolote jema. Mfanyie mambo mema mengi uwezavyo hatimaye utaubadili moyo wake. Usiwe mtu wa kulipiza kisasi bali uwe mtu wa upendo na kusonga mbele kwenye mafanikio yako. Hata kama ataendelea kukuchukia ipo siku ataujua ukweli halafu atakuomba msamaha mwenyewe.

Jambo la saba: Fanya vizuri zaidi. Kama mtu anakuchukia kwa kuwa unafanya vibaya kwenye jambo fulani, unatakiwa udhamirie kufanya vizuri zaidi. Anza kufanya vizuri zaidi mfano; darasani, kazini kwako, kwenye biashara, kwenye kilimo, kanisani n.k. Unapofanya vizuri zaidi humridhishi mtu yule  anayekuchukia bali pia inakusaidia wewe kupata uzoefu na kuboresha maisha yako.

Jambo la nane: Usipambane  kwa nguvu za giza, kaa vizuri na Mungu wako. Kama mtu anayekuchukia anatumia nguvu za giza kukudhuru, usihangaike kutafuta nguvu za giza ili upambane naye. Unatakiwa kukaa vizuri na Mungu wako maana tunajua kwamba ulozi na uchawi hauwezi kumdhuru mtu aliye kaa vizuri na Mungu wake. Tena ukikaa vizuri na Mungu wako, halafu mtu mwingine atumie nguvu za giza kukudhuru, hajui anachokifanya maana Mungu atamjibu kwa mapigo makali.

Unayo Safari Ndefu
Kumbuka nilivyokwambia, hakuna mbadala wa maisha yako, maisha yako ni yako wewe mwenyewe, kama utabaki unakatishwa tamaa na mtu kiasi kwamba unaacha kusonga mbele kwenye mafanikio yako, ujue kabisa unajiandalia maisha magumu. Usikubali mtu yeyote kwa namna yoyote ile akurudishe nyuma kwenye safari yako ya mafanikio. Ukikwama kwenye maisha yako hakuna atakayekusaidia zaidi zaidi watakucheka na kukuona huna lolote. Kama ni hivyo kwanini ukatishwe tamaa na mtu. Usikubali, pambana hadi kieleweke na unatakiwa kuweka msimamo wa maisha yako. Unatakiwa kusema “kila jambo acha litokee tu lakini kufanikiwa lazima”.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Top Servicare. Powered by Blogger.

Web Design

Popular Posts

INSTAGRAM FEED

@soratemplates

Blog Archive

About