Saturday, October 31, 2015

UNAPOIHARIBU NAFSI YAKO

Habari yako ndugu na rafiki yangu;
Ninakukaribisha katika tafakari yetu ya leo, ambapo nimekuwa nikikuletea makala hizi kwa lengo la kukusaidia pale unapokwama ili kwa pamoja tusonge mbele katika maisha yetu na lengo langu kubwa ni ili mimi na wewe tufanikiwe. Masomo haya ninayokuletea haya kusaidii wewe tu wala siandiki ili nikufundishe wewe tu, kati ya watu wanaofaidika zaidi na masomo haya ni mimi mwenyewe yananifundisha mambo mengi sana na yananisaidia mambo mengi mno. Huwa na kaa na kutulia naanza kuzisoma makala hizi nilizoziandika mimi mwenyewe 

halafu najifunza mambo mengi ambayo yananisaidia kila siku kwenye harakati zangu za mafanikio. Kwa sababu mafanikio ni vizuri kumshirikisha  mwenzako ndio maana nakushirikisha wewe ili upate kufaidika na hatimaye ufikie mafanikio yako. Mfano mzuri, mwezi wa tano mwaka huu (2015)  nilipata fursa moja ya kujiunga na rafiki zangu wanne ili tuanzishe ufugaji wa kuku. Nilikuwa natakiwa kuchangia shilingi milioni mbili kwenye mradi huo. Kwa wakati huo 

sikuwa na pesa yoyote wala sikujua nitapata wapi pesa hizo. Wakati natafakari hayo nikakumbuka makala moja niliiandika kipindi cha nyuma kidogo yenye kichwa cha habari; Jinsi Ya Kupata Chochote UnachokitakaHaraka haraka nikakimbilia kuisoma makala hiyo, mara nilipomaliza kuisoma nikapata akili nikaanza kuyatumia mafunzo niliyojifunza humo. Baada ya siku mbili nilipata milioni mbili. Nilishangaa sana ndipo nikaelewa kuwa makala hizi ninazoziandika sio kwa ajili yako tu bali pia kwa ajili yangu.

Mara nyingi sana ninapokumbana na tatizo au changamoto fulani huwa natumia makala zangu kama washauri wangu na zimenisaidia sana siku kwa siku. Hivi karibuni nilikuletea makala nyingine yenye kichwa cha habari; Kukiomba Msamaha Kila Kiungo Cha Mwili Wako Ni Siri YaAjabu Kukutoa Kwenye Tabia Sugu. Wakati naendelea kuyafanyia kazi mafunzo yaliyomo kwenye makala hiyo, nimekuja kugundua kwamba usiporekebisha baadhi ya mwenendo wa maisha yako hutaweza kamwe kujinasua na tabia sugu. Tabia sugu maana yake 

ni mwenendo na matendo ambayo umekuwa ukiyafanya, lakini hupendi uyafanye kwa sababu yanakuharibia maisha yako, tena yanakupotezea muda, kibaya zaidi yanakurudisha nyuma kwenye harakati zako za kuelekea mafanikio makubwa. Pamoja na ubaya wa hiyo tabia sugu kwako, bado huwezi kuiacha au unajaribu kuiacha lakini unajikuta umerudia tena. Mfano wa tabia sugu inaweza kuwa ni uvivu, unajitahidi uache uvivu lakini bado unashindwa kuacha, unajikuta unaendelea kulala au kupiga soga mpaka muda wa kufanya mambo mengine ya maana unaisha halafu unajisemea nitafanya kesho na kesho ikifika yana kuwa ni yale yale tu. Tabia sugu inaweza kuwa ni uvutaji sigara unajitahidi 

lakini bado unashindwa kuacha kuvuta sigara.  Inaweza kuwa ni ulevi, unajitahidi uache kunywa pombe lakini unashangaa  umerudia kunywa pombe na unalewa vile vile, japo unapoteza fedha nyingi  ambazo ungezitumia kwenye shughuli nyingine za maendeleo. Inaweza kuwa ni uzinzi, unajitahidi uache lakini unajikuta huwezi kuacha, unaendelea kujilaumu na kujichukia lakini bado tu unafanya, hata hujui utatokaje. Inaweza kuwa ni kuangalia picha za ngono, unajitahidi uache lakini huwezi, ukibaki peke yako tu chumbani na simu au computa yako tayari unahamasika kuangalia picha za ngono na huwezi kujizuia. Tabia sugu inaweza kuwa ni kutotii ratiba yako uliyojipangia, kila mara unajitahidi uamke saa fulani ufanye kazi hii na hii lakini bado unashindwa kufanya hivyo. Hizo ni baadhi tu ya tabia sugu kwa kuzitaja. Wewe mwenyewe unajua tabia sugu yako ni ipi ambayo imekuwa inakusumbua siku nyingi na huipendi lakini ndo hivyo imekunasa.

Katika makala hii; KukiombaMsamaha Kila Kiungo Cha Mwili Wako Ni Siri Ya Ajabu Kukutoa Kwenye Tabia Sugu (kama hujaisoma naomba uisome itakusaidia), nilielezea mambo makubwa mawili yanayoharibu nafsi ambayo ni uzinzi na maneno. Lakini pia nilielezea uhusiano kati ya mwili, nafsi na wewe (maana wewe sio mwili lakini unaishi ndani ya mwili). Nikasema unapokuwa na mahusiano mabaya kati yako na mwili maana yake anayewaunganisha ili muelewane (translator) ambaye ni nafsi amejeruhiwa au amekufa kabisa. Kufa kwa nafsi maana yake imeshindwa kufanya kazi yake kisawasawa. Sasa ili nafsi yako irejee kwenye hali yake ya kawaida ni lazima kuiponya na njia mojawapo ya kuiponya nafsi ni kwa njia ya kuiomba msamaha. Baadaye nitakupa njia zingine.

Nini Kinakusumbua? Unafikiri Ni Kwa Nini?
Mahangaiko yoyote yanayokupata hasa ya moyoni chanzo chake ni kimoja tu ni kuilisha nafsi chakula kisicho sahihi. Nafsi hula chakula kupitia macho, masikio, maneno (ulimi), ngozi nk. Hivi viungo nilivyovitaja kila kimoja kwa nafasi yake na kwa wakati wake hupeleka chakula kwenye nafsi, kama chakula ni sahihi utaisikia nafsi ikifurahi, lakini kama chakula sio sahihi utaisikia nafsi ikihuzunika na kukosa amani halafu unapata mahangaiko mengi moyoni. Mambo yoyote 

yale yanayoihuzunisha nafsi maana yake yanaijeruhi au yanaiua nafsi yako. Hebu fikiria ni kitu gani ambacho kimekuwa kikikuhuzunisha au kukukosesha amani mara kwa mara?. Hebu fikiria chanzo cha kuhuzunika huko ni nini? Je, ni wewe mwenyewe kwa tabia yako sugu au chanzo chake ni nje kabisa ya wewe?. Kama chanzo cha mahangaiko yako ni nje ya mwili wako mfano umesikia ndugu yako anaugua sana, gafula unapata huzuni hiyo chanzo chake ni nje yako na ni vigumu kuyaepuka mambo hayo na wala sio lengo langu kuyazungumzia hayo kwenye makala hii. Lakini kama chanzo cha huzuni yako ni wewe kutokana na tabia yako, basi fanya mambo haya manne yatakusaidia.

Jambo la kwanza: Acha kuilisha nafsi chakula chenye sumu. Chunga macho yako yasitazame mambo usiyoyapenda vinginevyo nafsi itakula sumu. Chunga maneno unayoyatamka pia kuwa makini na maneno unayoyasikia kama uko kwenye eneo lenye maneno usiyoyapenda ondoka haraka sana. Mfano mwingine, kama unapenda kuangalia miziki ya watu wakicheza uchi hapo unaiua nafsi yako, kwahiyo huwezi kujizuia kufanya uzinzi, kama sio uzinzi basi utapiga punyeto. Kwanini itakuwa hivyo? kwa sababu nafsi inakuwa imejeruhiwa haifanyi kazi yake kawaida. Bila kuiponya nafsi uwe na uhakika hiyo itakuwa tabia sugu kwako na hutaweza kuiacha mpaka umeacha kuilisha nafsi chakula chenye sumu.

Jambo la pili; Fanya juhudi za kujipatanisha wewe na mwili wako. Njia pekee iliyodumu vizazi vingi ya kujipatanisha ni kupitia kuomba msamaha. Iombe msamaha nafsi yako, na kila kiungo cha mwili wako ulichokitumia kufanya uovu. Dhamiria kuacha uovu na tumia njia hii ya kuomba msamaha itakusaidia sana, yaombe msamaha macho yako, ulimi wako, miguu yako, mikono yako na kila kiungo ulichotumia kufanya uovu.

Jambo la tatu: Kaa mbali na marafiki wanaokurudisha nyuma. Usijidanganye kwamba nitakuwa nao tu lakini nitakuwa najiepusha na matendo yako. Kumbuka kuna msemo usemao;  “je, unaweza kuweka kaa la moto kifuani na nguo zako zisiungue?” Au “je, unaweza kukanyaga kaa la moto na nyayo zako zisiungue?”. Kuwa makini na hilo, kumbuka hata maneno unayoyasikia yanaweza kuharibu nafsi yako.

Jambo la nne: Usijaribie kufanya uovu eti kwa kisingizio kwamba sasa nimeshajua niko makini sitafanya. Hapo unajidanganya tu, lazima utafanya kama sio leo utafanya kesho kwa kisingizio hicho hicho cha kujaribia tu.

Usipoyazingatia Hayo Kuna Madhara Yoyote?
Usipoyazingatia hayo hutafanya kile unachokitaka, lazima utafanya usiyoyataka halafu utaendelea kuumia moyoni mwako siku zote. Kama una kazi ya kutumia akili, ufanisi wako kwenye kazi hiyo utakuwa mdogo kwa sababu ya kuhuzunika na kujuta. Ni vema ukayazingatia ikiwa unataka kuishi maisha mazuri yenye furaha na amani na mafanikio.

Ushauri Wa Mwisho Kwenye Swala Hili.
Soma kitabu hiki The mastery of loveKitakusaidia kushinda kila tabia sugu inayokusumbua. Nakutakia utekelezaji mwema na Mungu akusaidie uvuke kwenye mahangaiko hayo.

“Tabia sugu maana yake ni mwenendo na matendo ambayo umekuwa ukiyafanya, lakini hupendi uyafanye kwa sababu yanakuharibia maisha yako, tena yanakupotezea muda, kibaya zaidi yanakurudisha nyuma kwenye harakati zako za kuelekea mafanikio makubwa”

Tunakuhamasisha Ili Ufikie Mafanikio Yako
Share:

0 comments:

Post a Comment

Top Servicare. Powered by Blogger.

Web Design

Popular Posts

INSTAGRAM FEED

@soratemplates

Blog Archive

About