Wednesday, November 4, 2015

Una Uwezo Mkubwa Na Akili Za Kufanya Kile Unachotaka, Vitumie

Habari  mpenzi msomaji wa TOPSERVICECARE. Ni matumaini yangu kuwa mpo salama , ni wakati mwingine tena tunakutana kwa ajili ya kuzidi kujifunza na kukumbushana namna sahihi ya kuangalia mambo. Ndugu yangu napenda nikukumbushe kuwa wewe umeumbwa ukiwa na uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo, ulipewa akili na uwezo wa kufanya kile unatakiwa kufanya hapa duniani.
UNAWEZA.
  
Kuna wakati unakutana na mambo ya kusikitisha na kuumiza pale ambapo mtu anakuwa kama amezipeleka akili zake likizo, au naweza sema amejisahau au kujipoteza kabisa , haelewi hata ni nani, anaenda wapi?, kwa nini yupo? n.k. Baadhi ya watu wapo tu kwa kuwa wapo. Baadhi ya watu hawaelewi hata uwezo walio nao, hawajui kusudi la wao kuwepo hapa duniani, mwingine anafikiri alikuja hapa ili aishie kutamani kuwa kama wengine, hajui kama naye ikiwa atatembea na kukaa kwenye ile nafasi yake anacho kitu cha maana , cha 



kumfanya na wengine watamani kuwa kama yeye, japo ukweli ni kwamba hakuna mtu awaye yote duniani hapa anaweza kuwa kama wewe ndugu yangu, wewe ni wewe, ni wa peke yako, uliumbwa hivyo kwa kusudi maalumu, Kama ulikua haujui hilo ndio nimekujulisha leo na ikiwa ulisahau basi nakukumbusha tu kuwa hakuna aliye kama wewe, usijifananishe na mwingine wala usitamani kuwa kama yule maana hauwezi kuwa vile, utakuwa unajichosha na kujichelewesha kufika kule unaenda tu, tafuta na tamani kuwa kama wewe yule Muumba alikukusudia uwe, tafuta kujua na kuona ule uwezo umeumbwa nao ndugu yangu, tambua zile akili umepewa ndugu yangu. 

Ni jambo la kusikitisha pale unapokutana na mtu anasema kwa kujiamini kabisa kuwa hawezi kufanya jambo fulani na ukitaka kujua ni kwa nini atakuambia eti kwa kuwa fulani alijaribu akashindwa, yaani kwa kuwa tu yule alishindwa naye anaamini atashindwa, anakubali kushindwa bila hata kujaribu kufanya kile kitu, anajipima kwa kumwangalia mtu yule, anajiona yeye hawezi kufanya zaidi ya yule, ndugu yangu tambua kuwa katika maisha haya usitumie kushindwa kwa mwingine kama kipimo cha kwamba nawe huwezi kwenda zaidi ya pale, kwamba hauwezi kufanya zaidi yake, tambua utofauti uliopo miongoni mwetu wanadamu wote, tuna uwezo tofauti wa kufanya mambo, hata namna ya kufikiria tunatofautiana. 




Mwingine anashindwa kwa kuwa tu kachagua kushindwa, ninasema kachagua kushindwa kwa maana ya kwamba kama mtu unatumia kigezo cha kwamba kama na yule kashindwa basi na mimi siwezi, mtu huyu ameamua na kuchagua kushindwa lakini angeamua kuangalia kushindwa kwa mwenzie kwa namna tofauti angeweza kufanya vizuri zaidi. Badala ya kukubali kushindwa kwa kuwa yule kashindwa au alishindwa unaweza kuamua kumfuata yule aliyeshindwa na uweze kuchunguza na kuelewa ni kwa nini alishindwa na kuanzia hapo unaweza kupata vitu vya kukufanya wewe hata ukiamua kufanya hilo ufanye kwa uzuri na usahihi zaidi, maana unajua wapi mwenzio aliangukia, unakuwa na nafasi ya kurekebisha. 

Lakini pia ukitambua kuwa wanadamu tunaomba mambo yale yale kwa utofauti hautalinganisha uwezo wako na wa yule, utatambua kuwa wewe ni wewe na yule ni yule, lakini ukielewa kuwa muumba wako amekupa uwezo , akili na nguvu za kufanya kile anataka ufanye hautajilinganisha na wengine, hautajipima kwa kuangalia yule kafanya nini. Maana cha muhimu ni wewe kutambua uwezo wako, nafasi yako na kusimama hapo, kufanya kila jambo kuendana na nafasi yako, kujiona wewe kama wewe na kuona kuwa unao uwezo wa kufanya kile umeumbwa uje kufanya, ni vyema kuuliza, kuomba ushauri kwa wengine lakini katika hayo usisahau akili zako, au kuna ule usemi unasema ukiambiwa changanya na zako, pima , jihoji angalia kama ni kweli, kinafaa kwako, usiwe ni mtu wa ndio kila wakati, chunguza mambo, pima, amua. 



Ndugu yangu hata ukiambiwa kitu usiwe ni mtu wa kukubali tu, kubali ikiwa kweli kinakubalika na una sababu ya msingi ya kukubali ikiwa kinyume kuwa mkweli na uonyeshe kile unaona na kuamini, usiogope kusema ukweli, usiogope kusimamia kile akili yako inakuridhisha kuwa ni kweli na sahihi hata kama hakuna mtu anayekuelewa lakini ikiwa dhamiri yako haikuhukumu uwe na amani na kusimamia hapo, usifanye jambo kwa kufuata mkumbo, fanya kwa kuwa una uhakika ndicho kitu unahitaji na ni kitu sahihi. 


Share:

ZIJUE FAIDA NNE ZA KUJENGA NYUMBA KWA KUTUMIA RAMANI YA NYUMBA


Ramani ni neno lililozoeleka masikioni mwa watu wengi kwa waliosomea fani hiyo ya ramani na hata kwa watu ambao hawajasomea fani hiyo kutokana na ukweli kwamba ramani hutumika kila siku katika maisha yetu ya kila siku na hakuna uwezekano wa kulipinga hili.

Mfano: Wewe ni mwenyeji katika eneo fulani na unamfahamu mzee mmoja katika eneo hilo anaitwa Mzee Mwamba, basi mara ukakutana na mtu mmoja akakauulizia kuhusu mzee huyo na akakuomba umwelekeze mahali anapoishi mzee huyo, bila shaka utaanza kumwelekeza: nyooka na barabara hii kama mita hamsini hivi mbele utaona barabara inakunja kona kuelekea kulia nenda nayo hiyo barabara kama mita miambili hivi utaona jengo kubwa jeupe mkono wa kushoto halafu mkabala na jengo hilo utaona  duka la vifaa vya ujenzi, uliza hapo dukani watakuonesha nyumba ya huyo mzee.


Hayo maelekezo uliyoyatoa ni ramani sema tu hujaichora na ukiamua kuichora utaiona kama zilivyo ramani za kawaida.
Kwa mantiki hiyo kila mtu kichwani mwake ana ramani nyingi sana nzuri zenye manufaa kwake na kwa taifa kwa ujumla na laiti ramani hizo zingechorwa  tungekuwa na maktaba kubwa ajabu na wakati mwingne hata sehemu ya kuhifadhi zisingetosha.

Maisha ya kila siku.
Unapotaka kuishi kwako yaani katika nyumba yako mwenyewe kuna ramani ya nyumba yako ungependa iwe yaani mwonekano, rangi, ukubwa na hata mwelekeo (orientation) wake. Ungependa umpate mtu mwenye uwezo wa kuionesha ramani hiyo iliyoko kichwani mwako na kisha uipate na uanze hatua  ya kuijenga ili uipate ile furaha unayodhani utaipata mara nyumba hiyo itakapo kamilika.



Itakusaidia kukadria gharama za ujenzi.
Maadamu  ramani hiyo itakuwa imeonesha vipimo vya “material” ya ujenzi itakuwa rahisi kujua idadi ya bati, matofali, madirisha,nk hii itasaidia kukufanya ujipange vizuri kabla ya kuanza ujenzi.

Ni kiambatisho muhimu katika kupata kibali cha ujenzi.
Kwa mujibu wa sheria ya ujenzi wa majengo  inataka ili mtu apate kibali cha ujenzi wa jengo lolote ni lazima aambatanishe katika maombi yake ramani ya jengo analotaka kujenga. Ramani hii itasainiwa na Afisa mipango miji, afisa ardhi na bwana afya na kamati ya ujenzi ya wilaya/mji/manispaa/jiji. nk

Ramani ya nyumba ni kielelezo muhimu katika taasisi za mikopo.
Ukitaka kuchukua mkopo benki au katika taasisi za mikopo na hasa ukitaka kuweka nyumba kama dhamana watahitaji kuiona ramani ya nyumba yako na watahitaji kuiambatanisha katika barua yako ya maombi ya mkopo huo.

Hizo ndizo faida kuu nne za kujenga nyumba kwa kutumia ramani ya nyumba ingawaje zinaweza kuwepo nyingine nyingi, ikumbukwe kuwa kujenga nyumba bila ramani ni sawa na kulima shamba kubwa bila kujua utapanda nini katika shamba hilo, ni hatarii.






TOPSERVICECARE tunaamini kuwa “Kile akili ya binadamu inakiwaza na kukiamini, akili ya binadamu inaweza kukipata”.Na tena, Mtu mmoja mwenye ujasiri ni watu wengi


Tunakuhamasisha ili ufikie mafanikio yako
Share:

NAMNA YA KUPATA KIBALI CHA UJENZI WA NYUMBA ILI USIJE UKAPIGWA STOP WAKATI WA UJENZI WA NYUMBA YAKO



Kutokana na kuongezeka kwa ujenzi holela sehemu za mijini, Serikali iliamua kuandaa sheria ya mipango miji inaitwa “Sheria ya Mipango Miji namba 8 ya mwaka 2007”. Sheria hiyo inaelekeza namna ya upangaji wa miji.  Moja ya maagizo ya sheria hiyo inamtaka kila mtu anayejenga nyumba kwenye eneo liliotangazwa kuwa eneo la mipango miji awe na kibali cha ujenzi na asipokuwa na kibali hicho hatua zaidi huchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa kujenga.
Kwa kufuata maagizo ya sheria hiyo kila halmashauri nchini huandaa sheria ndogo ndogo (by laws) za namna ya utoaji wa kibali hicho cha ujenzi. Sheria hizi ndogo ndogo  hutofautiana kutoka halmashauri moja hadi nyingine. Lakini angalau huwa kuna mlolongo unaokaribiana katika utoaji kibali hicho. Nachukua nafasi hii kukushrikisha mlolongo (hatua) za kupata kibali hicho.

Hatua ya kwanza: Andaa Ramani Ya Nyumba Utakayoijenga
Unatakiwa kuwa na ramani ya nyumba utakayo ijenga. Ramani unaweza kuipata kwa mtu yeyote anayechora ramani za nyumba mfano anaweza kuwa Msanifu ramani, au Msanifu Majengo anaweza kukuchorea ramani nzuri.



Hatua Ya Pili: Ramani Hiyo Inatakiwa Kuidhinishwa Na Msanifu Majengo (Architect) Aliyesajiliwa.
Lengo la Msanifu Majengo kuiidhinisha ramani hiyo ni ili kuangalia ubora na vigezo muhimu vinavyotakiwa kwenye nyumba. Pia likitokea tatizo kwenye nyumba hiyo Archtect atawajibika kujibu ikiwa tatizo hilo litatokana na kosa la mchoro wa nyumba hiyo. Wasanifu majengo waliosajiriwa wako wengi kwenye kila mkoa. Ulizia tu utawapata, kinachotakiwa Msanifu majengo huyo atapiga mhuri wake aliopewa na Bodi ya usajiri wa wasanifu majengo kwenye kila ukurasa wa ramani hiyo.
Huwa kuna gharama kidogo kwenye kuidhinisha ramani kwa architect kulingana na aina ya ramani, mfano kama ni ramani ya nyumba ya kuishi yenye vyumba vitatu au vine kuna wengine huwa wanafanya shilingi 50,000/= na wakati mwingine huwa zaidi ya hapo.

Hatua Ya Tatu: Chukua Fomu Kutoka Ofisi Ya Ujenzi Na Uzipitishe Zisainiwe Kila Sehemu Inayohitajika
Fomu hizi zinatakiwa zipitishwe kwa Afisa Ardhi wa Wilaya husika, kwa Afisa Mipango Miji na kwa Bwana Afya wa Wilaya. Sehemu hizo zote kila mmoja atakagua mambo yake. mfano, Afisa Ardhi atakagua kama kiwanja kinamilikiwa kihalali na kinalipiwa kodi ndio maana unatakiwa uambatanishe na Hati au Offer ya kumiliki kiwanja na risiti ya malipo ya kodi ya kiwanja ya hivi karibuni.

Afisa Mipango Miji atakagua aina ya nyumba unayotaka kujenga na matumizi yake na atalinganisha kwenye ramani ya mipango miji ajue eneo unalotaka kujenga hiyo nyumba linepangiwa matumizi gani. Kama eneo unalotaka kujenga limetengwa kwa ajili ya viwanda na wewe unataka kujenga nyumba ya makazi hata kubali kusaini kwenye sehemu yake. Bwana Afya atakagua ukubwa wa madirisha na uhusiano wa matumizi ya chumba kimoja na kingine. Pia atakagua shimo la maji taka (septic tank). Ukimaliza kupitisha huko utairudisha fomu hiyo ofisi ya ujenzi.

Hatua Ya Nne: Kutembelea Kiwanja Na Kujiridhisha.
Baada ya hapo Mhandisi wa Ujenzi itabidi uende naye kwenye kiwanja unachotaka kujenga ili akajaze taarifa za kiwanja chako na akajiridhishe kama kiwanja kweli kipo. Taarifa ya kiwanja chako atazijaza kwenye fomu hizo kuna sehemu ya kujaza Mhandisi wa Ujenzi. Halafu atapiga mhuri wa ofisi ya ujenzi kama ishara ya kwamba kila kitu kiko vizuri.

Hatua Ya Tano: Kuidhinishwa Na Kamati Ya Ujenzi Ya Wilaya Husika.
Mhandisi wa ujenzi akisha kagua kiwanja chako na akajaza taarifa zake kwenye fomu, kinachofuata ramani hiyo na fomu zote itapelekwa kwenye kikao cha kamati ya ujenzi ya Wilaya ambacho hukaa mara moja kila baada ya muda fulani mfano kuna baadhi ya halmashauri kamati hiyo hufanya kikao chake kila baada ya miezi mitatu. Kikao hicho ndicho kitaidhinisha kutolewa kwa kibali cha ujenzi wa nyumba unayotaka kujenga.

Hatua Ya Sita: Kibali Kinatolewa.
Mara baada ya kikao cha kamati ya ujenzi kumalizika, vibali vyote vilivyoidhinishwa kutolewa, hutolewa kwa wahusika. Kinachotakiwa wakati wa mchakato wote huo uwe na nakala 3 au 4 za ramani yako ya nyumba ili mara baada ya kutolewa kwa kibali cha ujenzi nakala moja atabaki nayo mwenye nyumba, nakala nyingine itapelekwa Ofisi ya Ardhi ya wilaya na nakala moja itabaki kwenye Ofisi ya Ujenzi kama kumbukumbu.
Ukipata kibali chako unaweza kuendelea na ujenzi wako kwa amani bila bughuza. Kutokuwa na kibali cha ujenzi ukibainika unaweza kuzuiliwa kujenga (stop order) mpaka utakapopata kibali cha ujenzi.


“Moja ya maagizo ya sheria hiyo inamtaka kila mtu anayejenga nyumba kwenye eneo liliotangazwa kuwa eneo la mipango miji awe na kibali cha ujenzi na asipokuwa na kibali hicho hatua zaidi huchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa kujenga

Tunakutakia kila la heri katika ujenzi wa Taifa. TOPSERVICECARE
Share:
Top Servicare. Powered by Blogger.

Web Design

Popular Posts

INSTAGRAM FEED

@soratemplates

Blog Archive

About